
Mwanafunzi wa Chuo mkazi wa Watumishi House Kata ya Mkundi Manispaa ya Morogoro aitwae Christian Joseph (19) amehukumiwa miaka 20 Jela kwa kosa la shambulio la aibu kwa mtoto wa kike wa miaka 5 (jina limehifadhiwa)
Tukio hilo lilitokea Septemba 9, 2023 maeneo ya Watumishi House Kata ya Mkundi Manispaa ya Morogoro baada ya Mshtakiwa kumuita sebleni kwao mtoto huyo anayeishi jirani na nyumba yao kisha kumvua nguo na kumtendea kitendo hicho cha kikatili.
Christian alikamatwa na Polisi siku ya tukio na kufikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Morogoro Oktoba 31, 2024 baada ya upelelezi kukamilika na kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 Jela chini ya Hakimu Ester Ushaki.
Akiongea kuhusiana na tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama amesema, kwa upande wa Jeshi la Polisi wataendelea kukamata, kupeleleza na kuwafikisha Mahakamani wale wote watakaobainika kufanya vitendo vya Ukatili kwa watoto.
Aidha, ameitaka jamii kutoa taarifa ya vitendo hivyo ili wahusika wakamatwe na kuchukuliwa hatua stahiki iwe mfano kwa watu wengine.
Kamanda Mkama amekemea wale wote wanaosuluhisha kifamilia matukio ya ukatili kwa sababu ya kuoneana muhari.


