Na Saada Almasi, Itilima – Simiyu.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilayani Itilima Mkoani Simiyu, imemhukumu kifungo cha miaka mitatu jela Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Sunzula B iliyopo Wilayani humo, Bahati Suguti kwa kukutwa na hatia ya kusaidia Wanafunzi wa Darasa la nne kufanya udanganyifu wa mitihani akiwa na wenzake watano.
Mwalimu Suguti na wenzake walishtakiwa kwa makosa mawili ikiwemo la kula njama ya kutenda kosa kinyume na kifungu cha 384 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2016 na kufanya udanganyifu kinyume na kifungu cha 23 na 24 vya sheria ya baraza la mitihani sura ya 107 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019 pamoja na kanuni ya 16 (11)(c) ya kanuni ya mtihani ya mwaka 2016 kama ilivyotangazwa na kwenye gazeti la serikali namba 89 la mwaka 2016.
Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mashtaka Wilaya ya Itilima ambaye ni Mkaguzi wa Polisi, Jaston Mhule amedai kuwa Oktoba 25, 2023 katika shule ya Msingi Sunzula B, washtakiwa Bahati Suguti, Stephano Daudi, Fauzia David, Mwita Boniface, Masatu Jepharine na Salome Aaron walitenda kosa la kula njama na kusaidia wanafunzi wa darasa la nne kutenda kosa udanganyifu katika vyumba vya mtihani.
![](https://jambofm.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/Screenshot_20250210-203313_Google.jpg)
Hukumu hiyo ya shauri la jinai namba 27062/2024 iliyosikilizwa na kutolewa hukumu na hakimu mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Itilima, Robert Kaanwa upande wa mashtaka ulikuwa na jumla ya mashahidi tisa na vielelezo 4 bila kuwa na mashahidi upande wa washtakiwa ilijiridhisha pasi na shaka kuwa Mwl. Suguti amehusika moja kwa moja na kosa la kuwasaidia Wanafunzi kufanya udanganyifu katika vyumba vya mitihani na kuwaachia huru wenzie watano.
Baada ya kutiwa hatiani upande wa mashtaka uliomba mshtakiwa apewe adhabu kali, ili iwe funzo kwake na kwa jamii kutokana na madhara kwa jamii na kugharimu Serikali gharama za uratibu wa mitihani lakini pia kupelekea wataalamu ambao hawatoi mchango chanya katika jamii.
Mshtakiwa aliomba mahakama impunguzie adhabu kwani ni kosa lake la kwanza na ana familia inayomtegemea na ni mtumishi wa Serikali ndipo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo Robert Kaanwa akamhukumu adhabu ya jela miaka 3 au kulipa faini ya shilingi milioni 5 na alishindwa kulipa faini hiyo hivyo kupelekwa jela.