MWALIMU ALIYELAZWA KWA KIPIGO AKIDAIWA KUCHELEWA SHULENI ASIMULIA TUKIO

Mwalimu wa Shule ya Sekondari (JSS), iliyoko Nyamira Nchini Kenya, Vincent Onyancha ambaye alilazwa Hospitalini kwa kudaiwa kupigwa na Mwalimu Mkuu wake amekanusha madai kwamba alienda darasani akiwa mlevi.

Onyancha ameyasema hayo katika mahojiano na Wanahabari na kudai kuwa yeye hunywa pombe wakati hayuko kazini na si mara nyingi kwa sababu ya ugumu wa maisha.

Mwalimu huyo wa eneo la Bunge la Mugirango Kaskazini, amesema pombe haijawahi kuathiri utendakazi wake na kudai kuwa wiki jana, Ijumaa ya Februari 21, 2025, alifika kazini akiwa amechelewa.

Mwalimu wa Shule ya Sekondari (JSS) Nchini Kenya, Vincent Onyancha.

Amesema, “nilifika na nikaongoza moja kwa moja hadi chumba cha walimu na kuchukua vitabu na vifaa vingine na kuelekea darasani tayari kwa somo na wanafunzi wangu. Nilipoanza kufundisha Mwalimu Mkuu alijitosa darasani na kuanza kuniangushia makofi mazito mazito.”

“Nilikuwa nimefika tu darasani na nimekwisha tulia alipoingia kwa nguvu. Aliniuliza kwa nini nilichelewa kufika shuleni. Kabla hata sijatoa maelezo, alinishukia kwa mateke na makofi. Alinivuta nje ya darasa huku wanafunzi wangu wakitazama kwa mshangao,” alisema Onyancha.

Ameendelea kusimulia kuwa, “alinipiga bila huruma. Aliniangusha sakafuni katika afisi yake na kunikanyaga mgongoni. Nilijaribu kujieleza lakini hakusikia lolote. Sikuaibika tu mbele ya wanafunzi wangu bali pia machoni pa walimu wenzangu.”

Vincent Onyancha, mwalimu anayedai kupigwa na mwalimu mkuu wa shule anakofundisha Nyamira. (Picha|Wycliffe Nyaberi)

Kufuatia tukio hilo, Onyancha ameitaka Tume ya Huduma na Uajiri wa Walimu (TSC) na mamlaka zote husika kuchunguza kesi yake kwa kasi na kuchukua hatua zinazofaa.

Kwa upande wao Wasimamizi wa Hospitali ya Medstops alipokuwa amelazwa mMwalimu huyo, walikataa kufichua kiwango cha majeraha aliyoyapata, wakidai kufanya hivyo kunaweza kuweka kituo hicho katika hali mbaya.

Mmoja wa Wasimamizi hao alisema, “sitaki kuzungumzia sana suala hili kwa sababu linachunguzwa na asasi nyingi. Kuna mengi yanazungumzwa kuhusu mwalimu huyo na kwa hivyo, tungependa kutozungumza zaidi.”

credit – taifaleo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *