Kesi dhidi ya bondia wa ngumi za kulipwa Nchini, Hassan Mwakinyo ambayo imefunguliwa na Kampuni ya PAF Promotion inatarajia kutajwa kwa mara ya kwanza Novemba 13, 2023 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, A.H. Msumi ikiwa na jumla ya madai 8 ya msingi, ikiwa ni Pamoja na Mwakinyo kuilipa kampuni hiyo milioni 142.5 kutokana na hasara ya kukosa mapato iliyotegemea kutoka kwa wadhamini.
Kampuni hiyo imewasilisha madai hayo kupitia wito wa kesi uliotolewa na Mahakama ambapo PAF imeiomba Mahakama itamke kwamba bondia huyo amevunja mkataba wa kupigana.
Madai ya tatu, PAF imeiomba Mahakama kumtaka Mwakinyo aombe radhi kwa kuichafua kutokana na kutoa taarifa za uongo kupitia Vyombo vya Habari alivyotumia kuichafua Kampuni na Wakurugenzi wake.
Madai ya nne, imeiomba Mahakama kumtaka Mwakinyo arejeshe fedha Dola za Marekani 3,000 alizopewa kuelekea pambano hilo alilotakiwa kupigana. Madai ya tano, PAF imeomba kurejeshewa Shilingi Milioni 8 yakiwa ni malipo ya kulipia ukumbi.
Madai namba sita, PAF imeomba kurejeshewa Shilingi 1,287,500 ikiwa ni gharama za malazi ya mpinzani wa bondia huyo.
Madai namba saba, PAF imeomba kurejeshewa Shilingi 3,832,000 ambayo ni gharama za tiketi za ndege za mpinzani wake pamoja na Wasaidizi wake.
Aidha, mbali ya madai hayo, PAF kupitia wakili wake, Herry Kauki wa Kampuni ya Wakili ya Shepron Attorneys ya Dar es Salaam, imeomba Mahakama kulipwa jumla ya Shilingi milioni 150 ikiwa ni madhara ya jumla waliopata baada ya bondia huyo kushindwa kupanda ulingoni tofauti na mkataba wake aliosaini.