MVUA YALETA MADHARA MUSOMA, JENGO LA HISTORI LAHARIBIWA

Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali, iliyonyesha hivi karibuni katika kijiji cha Mkirila wilayani Musoma mkoani Mara, imeezua na kubomoa nyumba zaidi ya 20 pamoja na kuharibu vibaya jengo la asili la kabila la Wakwaya, lililojengwa mwaka 1957 na kutumiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika harakati za kudai Uhuru.

Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Mkirila, Julius Mjengwa amesema, mvua hiyo ilikuwa na nguvu kubwa na ilisababisha athari kwa kaya zaidi ya 20, ambapo familia kadhaa zimelazimika kutafuta makazi mbadala.

Licha ya madhara kwa makazi ya Wananchi, wakazi wa Kijiji hicho wamesikitishwa zaidi na uharibifu uliofanywa katika jengo hilo la kihistoria lililowahi kuwa ofisi ya kwanza ya Mwalimu Nyerere katika eneo la Bukwaya na Majita.

“Kahiyo mimi nalilia hii nyumba kwa kuwa Mwalimu Nyerere alituachia hapa. Kihistoria, hii ndiyo ilikuwa ofisi ya kwanza kutumiwa na Mwalimu katika eneo hili lote la Bukwaya na hata Majita,” amesema mzee Belius Mranda, mmoja wa wazee wa mila.

Kwa upande wao, Viongozi wa eneo hilo wameiomba Serikali na Wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia ukarabati wa jengo hilo, ili kuzuia historia yake kupotea kabisa.

“Jengo hili lilijengwa na kufunguliwa na Mwalimu Nyerere mwaka 1957, na lilitumika sana katika vikao na mikakati ya kudai Uhuru. Tayari tumewaarifu viongozi wa ngazi za juu kuona namna ya kunusuru historia hii kabla haijatoweka,” ameeleza John Kilasangi, kiongozi wa Kata ya Nyegina.

Wakazi wa Mkirila wanaamini kuwa kukarabatiwa kwa jengo hilo kutadumisha urithi wa kihistoria wa jamii ya Wakwaya na kulinda kumbukumbu muhimu za harakati za ukombozi wa taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *