MVUA YAISUBIRISHA TANROADS KUKARABATI BARABARA SINGIDA

Na Saulo Stephen – Singida.

Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mkoa wa Singida imsema inasubiri kupita kwa Msimu wa Mvua unaoendelea katika maeneo mbalimbali, ili kuanza zoezi la ukarabati na Matengenezo ya Barabara zilizopo Katika Mkoa wa Singida.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida, Mhandisi Dastan Singano leo Februari 26, 2026 wakati akizungumza na Jambo Media Ofisini kwake Mjini Singida.

Amesema, katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha katika Maeneo mbalimbali Nchini ikiwemo Mkoa wa Singida inakuwa ni vigumu kupeleka mitambo kwenye maeneo ya barabara zinazohitaji kufanyiwa marekebisho na Metengenezo.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida, Mhandisi Dastan Singano.

Amewaomba wananchi wote katika Mkoa wa Singida ambao wanakumbana na adha miundombinu ya barabara isiyo rafiki, kuwa wavulivu katika kipindi hiki na kuahidi kuwa punde msimu wa Mvua utakapokamilika, TANROADS Mkoa wa singida wataanza kuzifanyia kazi barabara hizo ili wananchi weweze kufurahia upatikanaji wa barabara nzuri na imara.

Mha. Singano ameitaja barabara ya Kititimo – Makiungu inayokwenda Mpaka wilaya chemba mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa barabara ambazo zitakwenda kutengenezwa kwani kwa sasa wako hatua za mwisho kumpata mkandarasi kwa ajili ya matengenezo ya barabara hiyo.

“Lakini kwa Mipango ya Muda mrefu tumepokea maelekezo ya Muheshimiwa Rais ya kuijenga barabara ile kwa utaratibu wa PPP kwa kushirikiana baina ya wizara ya ujenzi na wizara ya uchukuzi, Wizara ya Ujenzi ikiwakilishwa na (TANROADS), huku wizara ya uchukuzi ikiwakilishwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ili kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo inayoanzia Handeni Mkoani Tanga” Amesema Mha. Singano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *