Na Tryphone Odace – Kigoma.
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema meli ya MV Liemba itaanza rasmi kutoa huduma za usafirishaji wa abiria kuanzia Septemba 1, 2026, baada ya kukamilika kwa ukarabati wake.
Prof. Mbarawa ameyasema hayo Agosti 15, 2026 mjini Kigoma, wakati meli hiyo ilipokuwa ikifanya jaribio lake la kwanza katika Ziwa Tanganyika.

Amesema, kukamilika kwa ukarabati wa MV Liemba na kurejea kwake katika huduma kutachochea shughuli za usafirishaji ndani ya Ziwa Tanganyika, huku serikali ikilenga kuimarisha usafiri wa majini na kuongeza ufanisi na uhakika wa safari katika Mkoa wa Kigoma.
“Dhamira ya serikali ni kutumia usafiri wa majini kufungua zaidi mikoa ya magharibi na kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa,” amesema Mbarawa.
Naye Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Edward Mabula amesema, mradi wa upanuzi wa Bandari ya Kigoma unahusisha ujenzi na uboreshaji wa sehemu ya gati.

Amesema, maboresho hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza utayari na ufanisi wa MV Liemba, katika kutoa huduma za usafirishaji.
Baadhi ya wadau na wafanyabiashara Mkoani Kigoma, wamesema kuanza tena kwa safari za MV Liemba, kutasaidia kukuza shughuli za kiuchumi na biashara katika maeneo yanayozunguka Ziwa Tanganyika.

Wamesema, kuimarika kwa usafiri wa majini kutarahisisha usafirishaji wa abiria na bidhaa, hivyo kutoa fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi wa Kigoma na maeneo mengine yanayohudumiwa na usafiri wa majini.
MV Liemba, ambayo imekuwa sehemu muhimu ya historia ya usafiri katika Ziwa Tanganyika, inatarajiwa kurejea katika huduma ikiwa ni hatua muhimu katika juhudi za serikali kuimarisha usafiri wa majini nchini.


