MUTASINGWA AAHIDI KUENDELEZA ALIPOISHIA BYABATO JIMBO LA BUKOBA MJINI

Na Clavery Christian – Kagera.

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukoba Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Muhandisi Joansen Mutasingwa ameendelea na ziara zake za kampeni na mikutano ya hadhara katika kata ya Kashai, akiwahakikishia wananchi kuwa ataendeleza yale mazuri yaliyobuniwa na mtangulizi wake Wakili Stephen Byabato na kusimamia ujenzi wa miradi mipya ya kimkakati kwa maendeleo ya mji wa Bukoba.

Akizungumza katika mkutano mkubwa uliyofanyika katika uwanja wa soko la Kashai, mgombea huyo alisema Bukoba imepiga hatua kubwa katika sekta za huduma za kijamii, afya, elimu na miundombinu, jambo ambalo linapaswa kuendelezwa na kuwekewa msukumo mpya.

“Mtangulizi wangu alianzisha misingi imara ya maendeleo, kazi yangu itakuwa kuendeleza yale aliyoyaanza na kuongeza nguvu katika kuanzisha miradi mikubwa zaidi, ikiwemo uboreshaji wa barabara, maji, elimu, hospitali na uwekezaji wa viwanda vidogo na vya kati ili kuongeza ajira kwa vijana,” alisema Muhandisi Mutasingwa.

Aliongeza kuwa mpango wake ni kuifanya Bukoba kuwa mji mpya wenye sura ya kisasa kwa kuwekeza kwenye miradi ya kimkakati itakayokuza uchumi wa wananchi na kuchochea maendeleo ya Mkoa wa Kagera kwa ujumla.

Kwa mujibu wa ratiba yake ya kampeni, mgombea huyo anaendelea na mikutano katika kata nyingine za Bukoba Mjini akisisitiza amani na mshikikiano wa wananchi wote katika kufanikisha ndoto ya kujenga Bukoba mpya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *