Askari wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza wameaswa kushiriki na kusimamia vyema amani na usalama katika kipindi cha uchaguzi.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda amewataka Askari wa Jeshi la Polisi katika Mkoa huo kuimarisha amani na ulinzi hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linakwenda katika uchaguzi wa serikali za mitaa ili uchaguzi huo uweze kumalizika salama.
Mtanda ameyasema hayo wakati wa zoezi la kutoa hati, tuzo pamoja na pongezi kwa askari 9 wa askari wa jeshi la polisi Mkoa wa Mwanza waliofanya vizuri katika majukumu yao ambapo amesema zoezi la uchaguzi ni zoezi ambalo linatakiwa kufanyikwa kwa amani na utulivu hivyo ni lazima askari wa jeshi hilo kua mstari wa mbele katika kusimamia uchaguzi huo ili umalizike salama bila changamoto yoyote.
Aidha Mtanda amewataka askari hao kufanya kazi kwa nidhamu na weledi pamoja na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili waweze kutoa huduma bora kwa jamii.
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa amewapongeza askari wote waliopata zawadi hizo huku pia akisema zoezi hilo la kutoa zawadi linaenda sambamba na kutoa adhabu kwa askari wa polisi wanaoenda kinyume na maadili ya kazi hiyo.