MUSTAKABALI WA NCHI USIACHWE MIKONONI MWA VIONGOZI PEKEE – WANANCHI MARA

Baadhi ya wananchi mkoani Mara, wamesisitiza kuwa mustakabali wa amani na umoja wa Tanzania, hauwezi kuachwa mikononi mwa viongozi pekee, bali unapaswa kujengwa kupitia majukwaa ya wazi ya mazungumzo yanayowahusisha Watanzania wote.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika Manispaa ya Musoma, wananchi hao wamesema hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kuunda Tume ya kuchunguza matukio ya kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 2025 ni ishara ya mwanzo wa safari ya maridhiano ya kitaifa, lakini wakasisitiza kuwa hatua zaidi zinahitajika ili kuleta matokeo ya kudumu.

Wamesema tume hiyo iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman imefungua ukurasa mpya wa kusikiliza sauti za wananchi, lakini mafanikio yake yatategemea namna ambavyo majadiliano hayo yataendelezwa hadi ngazi za chini kabisa za jamii.

Kupitia maoni yao, wananchi hao wameeleza kuwa migogoro mingi nchini, ikiwemo ya kisiasa na kijamii, imekuwa ikichochewa na kukosekana kwa majukwaa salama ya watu kujieleza na kusikilizwa. Wanasema bila mazungumzo ya wazi na jumuishi, hata ripoti bora zinaweza kubaki makaratasi bila mabadiliko halisi.

“Ni wakati sasa wa Watanzania kukaa pamoja bila kujali tofauti zao za kisiasa, kidini au kikabila, na kuzungumza kwa uwazi kwa lengo la kujenga nchi moja yenye mshikamano,” amesema mmoja wa wakazi wa Musoma.

Aidha, wamewataka viongozi wa dini, wanasiasa na makundi mbalimbali ya kijamii kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha utamaduni wa majadiliano, wakiamini kuwa wao wana ushawishi mkubwa katika jamii unaoweza kusaidia kurejesha na kuimarisha imani miongoni mwa wananchi.

Wananchi hao wanaona kuwa maridhiano ya kweli hayaji kwa matamko pekee, bali yanahitaji vitendo vinavyojenga uaminifu, haki na usawa kwa kila Mtanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *