Mume,Mke Kizimbani kwa kuchakachua Wosia

Binti wa mmiliki wa kampuni ya Pelikan Signs Limited nchini Kenya aliyekuwa akisakwa na polisi kwa kughushi wosia ulioachwa na baba yao kwa lengo la kuwalaghai dada zake wawili amepandishwa kizimbani kujibu Mashtaka yanayomkabili.

Dinta Devani na mume wake Abhay Singh Pathiana walifika mbele ya hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani Bernard Ochoi wakiwa na wakili Danstan Omari aliyeomba radhi kwa niaba yao.

Kwa mujibu wa Maelezo ya wakili wao amedai Dinta na mume wake Abhay hawakujua kuwa walikuwa wanatakiwa kufika kortini kujibu mashtaka ya kughushi Wosia wa Balkrishna Harubhai Devani (babaye Dinta) na kurithi baadhi ya kampuni za familia yao kabla ya kupata taarifa kupitia mtandao wa Nation.Africa.

Awali Hakimu Mkuu Bi. Susan Shitubi aliagiza Dinta, Abhay na Addah Nduta Ndambuki wakamatwe kwa kujipatia kwa njia ya ulaghai hisa katika kampuni ya Pelikan Signs Limited.

Agizo la kuwatia nguvuni watatu hao lilitolewa wakati mkurugenzi mwingine wa Pelikan Signs Limited, Samuel Ndinguri aliposhtakiwa mbele ya hakimu huyo akikabiliwa na mashtaka matatu ya ulaghai na kujipatia hisa katika kampuni hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *