Na William Bundala, Kahama – Shinyanga.
Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoani Shinyanga kimewataka wananchi wa jimbo la Kahama hasa wale wenye nia ya kugombea Ubunge mwaka 2030, kutulia muda ufike na kumuacha Mbunge aliyepo, Benjamini Ngayiwa afanye kazi ya kuleta maendeleo kwa wananchi wa Kahama.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa katika mkutano wa hadhara uliandaliwa na Mbunge wa jimbo la Kahama mjini Benjamini Ngayiwa kwa lengo la kuwashukuru wananchi na kusikiliza kero zao.

Mlolwa amewataka wana Kahama kuacha maneno ya vijiweni ya kukatisha tamaa na kuanza kumfananisha Mbunge Ngayiwa na wapita njia wanaousaka Ubunge vijiweni ili hali mbunge aliyepo madarakani anatekeleza majukumu yake na chama cha Mapinduzi kimeridhishwa na utendaji wake.
“Sisi chama cha Mapinduzi tunaridhishwa na kazi anayofanya Ngayiwa,na mimi natetea kiongozi anayefanya kazi sitetei kiongozi mzigo hata kama ana pesa zake za kutosha,sasa wale wenye maneno maneno wanaotaka ubunge waambieni watulize mshono Muda bado na Ngayiwa ndio mbunge wa jimbo hili anayefanya kazi kisawasawa inayompendeza Mh.Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Mlolwa.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Ushetu Emmanuel Cherehani amewataka wananchi wa jimbo la Kahama mjini kutomuadhibu Ngayiwa kwa muda wa miezi mitatu aliyoapishwa kwa makosa ya watu wengine yaliyofanywa miaka 10 iliyopita na kuhaidi kushirikiana naye kupigania maendeleo ya Kahama.
“Niwaombe wananchi wa jimbo la Kahama achene kutumia madhaifu ya jimbo la Kahama kumsema vibaya mbunge wenu,msimuathibu Ngayiwa kwa makosa waliyofanya wengine kwa miaka kumi iliyopita,tupeni ushirikiano wabunge wenu wote wa majimbo matatu ili tuipiganie Kahama yetu kwa maendeleo ya vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema Cherehani.

Akizungumza kwenye mkutano huo wa kutoa Shukrani kwa wananchi, Mbunge wa jimbo la Kahama Mjini, Benjamini Ngayiwa amesema, hatovumilia kuona wananchi wa Kahama mjini wananyanyasika katika mambo mbalimbali kama kuondolewa kwenye maeneo yao wanapota ridhiki na kukosa huduma za maji na umeme pamoja na kero za barabara.
“Mimi sitovumilia kuona wananchi wa Kahama mjini wananyanyasika katika jimbo hili,marufuku kuwaondoa wananchi katika maeneo yao wanayopatia ridhiki pasipo kuwaambia mnawapeleka wapi,”

“Tunafahamu kero kubwa ya mji wa Kahama ni barabara sasa tumevunja mkataba wa mkandarasi aliyekuwepo na tarehe 1 mwezi wa 5 tunachoma nyama tule tukifurahia kupokea mitambo ya mkandarasi mpya anayekuja kujenga barabara zetu,” amesema Ngayiwa.
Ngayiwa pia amelipongeza Baraza la Madiwani Manispaa ya Kahama kwa kupitisha bajeti ya kununua mitambo ya kukarabati barabara ndani ya manispaa ya Kahama ambayo itasaidia kujenga kilometa mbili za rami kila mwaka.

Amesema, “nilishukuru sana baraza la madiwani Kahama mjini kwa kupitisha bajeti ya kununua mitambo ya kukarabati barabara,tumejiwekea utaratibu kila mwaka tujenge kilometa mbili za barabara za rami kila mwaka,hadi kuisha miaka mitatu Kahama itakuwa na miundo mbinu ya kisasa na barabara zenye taa kila kona.”
Katika mkutano huo wananchi wa jimbo la Kahama mjini wametoa kero zao huku nyingi zikiwa ni ardhi,barabara,maji na swala umeme ambazo kero hizo zilitolewa majibu na wakuu wa Idara wa sekta zote na kuhaidi kuyafanyia kazi.




