
Mwili wa mtoto wa mfanyabiashara maarufu Dodoma Zaituni Shabani Maarufu kama Jojo, aitwae Graison Kanyenye mwenye umri wa Miaka Sita umezikwa kwenye makaburi ya Kilimo kwanza yaliyopo Dodoma baada ya kukamilika kwa ibada iliyofanyika nyumbani kwao.
Mtoto Graison anadaiwa kuuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani wakati mama yake akiwa matembezini usiku wa kuamkia jana (Disemba 25).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi amesema kuwa tukio lilitokea saa 1.00 asubuhi katika Mtaa wa Bwawani, Ilazo Extension Kata ya Ipagala ambapo mwili wa mtoto huyo ulikutwa ndani ya nyumba ukiwa na majeraha shingoni.
“Kabla ya tukio hilo mtoto huyo aliachwa nyumbani majira ya saa Sita usiku na mzazi wake akiwa chini ya ungalizi wa Kelvin Gilbert ambaye ni bodaboda wa mtaa huo baada ya hapo mama mzazi wa mtoto huyo alirudi saa moja asubuhi na kukuta tayari mtoto ameuwawa,” amesema RPC Katabazi.
Katabazi amesema wanaendelea kumshikiria Kelvin Gilbert ambaye aliachiwa mtoto kwaajili ya uangalizi kwa uchunguzi zaidi juu ya tukio hilo ili kujua kilichosababisha tukio hilo.
Nae Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mlimwa Kusini Samwel Erasto ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao hasa katika kipindi hiki cha Sikukuu za mwisho wa mwaka.
“Nitoe wito kwa kina mama na dada hasa katika kipindi hiki cha sikukuu kuhakikisha wanawalinda watoto na hasa kuwa nao karibu ili majanga kama haya yasiweze kutokea na katika mtaa wangu hili ni tukio la kwanza halijawahi kutokea tangu nimeingia madarakani na hii ni awamu yangu ya pili tangu nianze kuongoza,”amesema.
Sambamba na hilo ametumia wasaha huo kulaani kitendo hicho na kutanabaisha kuwa kimeacha alama mbaya katika mtaa wao.
Moja kati ya majirani waliohudhuria katika msiba huo ni Elizaabeth Mwakikuti yeye amewasihi wazazi kuwa makini na watoto wao huku akiwakumbusha kuacha tabia ya kuwaacha hovyo hovyo kwani mtoto ni kitu chenye thamani kubwa.
“Yaani haiwezekani unaenda sehemu ya starehe au sehemu yoyote unamuacha mtoto mpaka anafanyiwa kitendo cha ukatili kama hiki yaani wazazi inabidi tujitafakari upya na hili tukio liwe funzo kubwa kwetu lisiwe la kuchukulia kawaida,”amesema Elizabeth.


