Costantine James,Geita
Mtoto Rashid Paul (6) aliyekuwa Mkazi wa kitongoji cha Ilyamchele katika kijiji cha Kabanga Kata ya Lulembela wilayani Mbogwe mkoani Geita amefariki dunia baada ya kuzama kwenye Bwawa la maji lililochimbwa kwa ajili ya shughuli za kilimo cha umwagiliaji katika eneo hilo wakati akivua samaki.
Akielezea tukio hilo baba mzazi wa marehemu amesema tukio hilo limetokea Agosti 30,2024 ambapo ameeleza kwamba mtoto wake kabla ya kukumbwa na mauti akiwa na watoto wengine walikwenda katika bwawa hilo wakati wakichunga mbuzi kabla ya kufikwa na umauti baada ya kuzama kwenye bwawa husika wakati akivua samaki.
Shuhuda wa tukio hilo Bw. Simoni Charles ambae alihusika kutoa mwili wa marehemu ndani ya bwawa hilo Amesema alipata taarifa ya tukio hilo baada ya kusikia sauti ya kelele za kuomba msaada kutoka kwa mama mmoja aliyekuwa akihitaji msaada wa kumuokoa mtoto huyo na alipofika alizama ndani ya bwa hilo na kutoa mwili wa marehemu.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Kabanga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kwamba tukio hilo ni la kwanza kutokea katika eneo lake na kueleza kwamba hatua iliyochukuliwa na serikali ya kijiji kuwaagiza wamiliki wa mabwawa ya kunyweshea mifugo na shughuli za umwagiliaji kuyawekea uzio ili kudhibiti matukio kama hayo.