Hali ya sintofahamu inazidi kuendelea kushika kasi ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) baada ya leo Aprili 5, 2025, Mwenyekiti wa Chama hicho, Tundu Lissu, kutengua uteuzi wa Mjumbe wa Sekretarieti ya Kamati Kuu ya chama hicho na Mtaalamu wa dawati la jinsia CHADEMA Catherine Ruge.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA Brenda, inaonyesha kutenguliwa kwa Catherine, ambaye jana alitoa tamko la kupinga uamuzi wa mwenyekiti wao kususia kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
“Mwenyekiti wa chama Taifa Tundu Lissu leo 5/4/2025 ametengua uteuzi wa Mjumbe wa Sekretarieti na Mtaalamu wa dawati la jinsia Catherine Ruge, Oparesheni ‘No Reform, No Election’ inaendelea kuchanja mbuga Kanda ya Kusini,” alisema Brenda.

Ndani ya Chadema kumekuwa na msuguano mkubwa baada ya jana makada na watia nia wa ubunge 55 wakijitokeza hadharani kupinga msimamo wa chama chao hicho, wakisema unakwenda kukiangusha chama kwa msimamo huo usiokuwa na faida kwa Chadema na Taifa kwa ujumla na kuikosoa taarifa ya ‘No Reforms, No Election’.
Makada hao ‘waliojiita’ G-55 wametuma waraka maalum kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika wakishauri chama hicho kuachana na kampeni hiyo badala yake wajiandae kushiriki uchaguzi kama ambavyo vyama vingine vilivyopo kwenye maandalizi kwa sasa, lakini waendelee kupigania mabadiliko huku wakiwa kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu.
