MTANDIO WAKATISHA MAISHA YA MWANAFUNZI SIMIYU


Na Sanda Almasi – Simiyu.

Msichana Latipha Juma (17), mkazi wa Kata ya Kidinda Wilayani Bariadi mkoani Simiyu amejinyonga kwa kutumia mtandio katika chumbani kwake usiku wa kuamkia Januari 30 2025 bila kuacha ujumbe wowote.

Latipha ambaye ni Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya Wasichana Simiyu inasemekana kabla ya umauti kumfika alikuwa na mama yake Happines Lushiba katika mlo wa jioni baada ya kuingia kulala na kutekeleza dhamira yake.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, mama mzazi wa binti huyo ambaye ndiye aliyemkuta mwanae akiwa amejinyonga asubuhi alipokuwa akimwamsha kwenda shule, amesema Latipha alihitaji kushonewa sare mpya za shule andapo angefaulu mtihani wa kidato cha pili cha kushangaza licha ya mama yake kutimiza ahadi yake bado hakumwambia kama kuna changamoto iliyokuwa ikimsumbua hadi kufanya maamuzi hayo.

Amesema, “aliniambia nimshonee nguo za shule na nikafanya hivyo alikwenda shule akiwa amependeza sana lakini sijui alikuwa na shida gani angeniambia tu maana nimekwenda kumuamsha asubuhi awahi shule nakuta tayari amejinyonga.”

Akizungumzia tukio hilo, Diwani wa Kata ya Kidinda, Kija John amesema Watoto wanapitia changamoto na mara nyingi wanaogopa kuzisema kwa mlezi ama mzazi hivyo ni jukumu la kila mmoja kutambua kuwa wapo viongozi na hata madawati ya kijinsia ambayo wanaweza kuzungumza nao na kupata suluhisho.

“Labda aliona mama mkali basi angeongea na baba yake lakini kama haitoshi angezungumza na viongozi lipo dawati la jinsia angesikilizwa tusingefika huku,kwa hiyo niwaombe wananchi wote wa kata hii tuwe na tabia ya kuzungumza matatizo yetu tusikae kimya,” alisema Kija.

Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoani Simiyu, Edith Swebe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa wataendelea kufuatilia, ili kujua chanzo cha tukio hilo na kutoa wito kwa jamii kujenga karibu na Watoto sambamba na kuzungumza nao, ili kujua changamoto wanazozipitia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *