Polisi kupitia Dawati la Jinsia na watoto wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, limewataka wananchi kuacha kuuza pombe za kienyeji kwenye makazi yao na badala yake ziuzwe kwenye maeneo maalumu ya kufanyia biashara hiyo.
Akieleza sababu ya katazo hilo leo Septemba 20, askari kutoka katika dawati la jinsia na watoto wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Veronica Fute amesema uuzaji wa pombe majumbani umekuwa ukiwasababishia watu wengi kesi za mauaji.
Ameongeza kuwa katika wiki hii ya kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia mkoani Simiyu, jeshi la polisi linaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa dawati la jinsia na watoto pamoja na kulitumia katika utatuzi wa migogoro ya ndoa.
Kampeni hiyo imezinduliwa mkoani Simiyu Septemba 18 mwaka huu ambapo malalamiko mengi ya ardhi yanayohitaji msaada wa kisheria yametolewa na baadhi ya wananchi ambapo wamesema maafisa wa ardhi wamekuwa wanachochea migogoro hiyo.
Akitoa ufafanuzi juu ya namna ya kumaliza migogoro ya ardhi katika jamii, Afisa Ardhi Mteule wa halmashauri ya mji wa Bariadi, Atupokile Mwandumbya amesema katika matumizi yoyote ya ardhi ni lazima wananchi wawashirikishe maafisa wa ardhi.