‘MSITUMIE MIHURI YA SERIKALI KUJIPATIA KIPATO ISIVYO HALALI’ – RC MACHA

NA EUNICE KANUMBA –SHINYANGA 

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, amewaonya wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji Halmashuri ya Shinyanga kuacha kutumia vibaya Mihuri ya Serikali waliyopatiwa ili kutoa huduma kwa wananchi bila kuendekeza masuala ya rushwa toka kwa wananchi na kujipatia mapato ambavyo siyo halali.

Macha ameyasema hayo leo Desemba 18,2024 wakati akifungua mafunzo ya Uongozi kwa Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga yaliyofanyika kwenye ukumbi wa shule ya wasichana Shinyanga iliyopo katika manispaa Shinyanga ambapo viongozi hao wamepewa miongozo ya namna ya kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

Macha amesema baadhi ya viongozi waliochaguliwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27,2024 ni wapya,hivyo wameona ni vyema kuwapatia mafunzo, ili wakawe wazalendo na waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na kutotumia mihuri vibaya na kuendekeza Rushwa.

“Nawapongeza kwanza kwa kuchaguliwa na wananchi,hivyo nendeni mkawe Wazalendo,na Waadilifu katika kuwatumikia wananchi na msitumie mihuri vibaya kwa kuendekeza Rushwa na kujipatia mapato ambayo siyo halali,” amesema RC Macha.

Macha amewataka pia Viongozi hao kusimamia amani na ulinzi katika maeneo yao ikiwamo kudhibiti uhalifu, kuhamasisha shughuli za maendeleo, uzalishaji mali,kusimamia mapato, kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia, kuzuia migogoro ya ardhi, pamoja na kutunza mazingira likiwemo suala la kusimamia usafi.

Mbali na hiyo, Viongozi hao pia wametakiwa kuhamasisha wananchi kujiunga na Bima ya Afya, matumizi na utumiaji wa vyandarua, ili jamii iwe na afya bora lakini pia ifikapo mwaka 2025 wasimamie zoezi la watoto kwenda shule hususani katika madarasa ya awali, Msingi na Sekondari, hii iende sambamba kutowaficha watoto wenye ulemavu ili nao wawapatie haki yao ya elimu.

Katika hatua nyingine,amewasisitiza viongozi wa Serikali za Mitaa kutoka CCM, kwamba washirikiane na viongozi waliochaguliwa kutoka katika vyama vya upinzani ili  wafanye kazi kwa pamoja ili kusukuma gurudumu la maendeleo.

Juma Tungu Mwenyekiti wa kitongoji cha Kasubuya kutoka CHADEMA, amesema mafunzo waliyopatiwa yatawasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao katika kuwatumikia wananchi.

Afisa uchaguzi kutoka Halmashuri ya wilaya ya Shinyanga Oscar Lupavila,ametaja takwimu kwamba wenyeviti wa vijiji katika Halmashuri hiyo wapo 126 huku wenyeviti wa vitongoji  wakiwa 856.

Aidha Lupavila ameanisha kuwa mada walizofundishwa katika mafunzo  hayo waliyopewa viongozi  ni sheria za uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, muundo, majukumu, madaraka ya vijiji,mitaa na vitongoji, utawala bora, maadili, uendeshaji wa vikao na mikutano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *