Jamii imetakiwa kuacha tabia ya kuozesha watoto ndoa za utotoni, kuachana tabia ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, vipigo kwa akina mama, huku wanandoa wakishauriwa kuacha kuishi kwa mazoea bila kuwa na cheti cha ndoa.

Elimu hiyo imetolewa kwa Wananchi wa Kijiji cha Wishiteleja Kata ya Mondo wilayani Kishapu, na Shirika linalotoa msaada wa kisheria mkoani Shinyanga Paralegal Aid Centre (PACESH), kwa ufadhili wa Shirika la WiLDAF kupitia Shirika la idadi ya watu la Umoja wa Mataifa UNFPA.
Meneja Miradi Shirika la PACESH John Shija, akizungumza katika utoaji wa elimu hiyo, amewataka wananchi wa Kijiji hicho kuacha kunyimana tendo la ndoa ili kuimarisha ustawi wa familia na kuishi kwa upendo na amani, na wanandoa kuacha tabia ya kuishi kienyeji bila ya kuwa na cheti cha ndoa, aidha cha kimila au kanisani.