MSIMU WA GANGAMALA: JAMBO FM YATETA NA SKAUTI IGUNGA

Ikiwa Radio Jambo Fm na Jambo digital tupo katika msimu wa Gangamala, msimu wa kukaza, msimu wa kuvuja jasho na damu kuhakikisha unafikia malengo yako, basi leo mwanaMaisha Fresh nimekuandalia story hii kuhusu chama cha skauti.

Skauti (kutoka neno la Kiingereza “scout”) ni mtoto au kijana anayewajibika katika chama, akivaa sare kama ya askari mdogo na kukaa katika mpangilio maalum.

Ni chama kisicho cha kiserikali kinachomjenga kijana katika maadili mema na ya kujituma na kusaidia watu katika maisha yao, kama anavyonieleza kamishna wa chama cha Skauti wilaya ya Nzega mkoani Tabora ndugu Hamdani Shemzigwa.

“Kwanza tunawagawa katika umri tofauti katika makundi manne ikiwemo ‘cub scout’ ambao ni vijana wadogo na tunakuwa na programu maalum kupitia shule za msingi na sekondari.” Amesema kamishna Shemzigwa.

SKAUTI ilianzishwa mwaka 1907 chini ya muasisi wake Robert Baden-Powell (1857–1941) kutoka Uingereza. Lengo lake lilikuwa kusaidia vijana kukua vizuri pande zote (mwili, nafsi na roho) ili hatimaye wawe raia wema katika jamii. 

Chama hiki kiliingia nchini kwa mara ya kwanza mwaka 1917 na baadae mwaka 1963 ndipo kulipisajiliaa rasmi na Tanzania kuwa nchi mwanachama wa Harakati za Skauti duniani.

Lakini ni vipi chama hiki kinawaandaa vijana kuendana na ulimwengu wa sayansi na Teknolojia tulionao kwa sasa? Ndugu Pascal Malole ni mratibu wa Skauti upande wa TEHAMA katika wilaya ya Nzega.

“Tuna utaratibu wa kuwapatia mafunzo ya kidigitali na tunaandaa ‘camp’ tofauti kwaajili ya mafunzo ya SKAUTI na katika kila matukio tuna utaratibu wa kurekodi matukio na kuyahifadhi katika mfumo wa kidigitali ili kusaidia vizazi vijavyo ndani ya chama Cha SKAUTI.” Amesema Pascal Makole. 

Nimezungumza pia na baadhi ya watoto ambao wengi wao wana umri chini ya miaka 16 wamenieleza ni kwanini wamevutiwa kujiunga na chama hicho cha Skauti.

“Naipenda SKAUTI kwa sababu inanifanya niwe mkakamavu na kuniandaa niwe mzalendo wa nchi yetu.” Amesema Clemensia Nikodemus

“Naipenda SKAUTI kwasababu inaniandaa kukabiliana na maisha yangu ya Sasa na ya baadae.” Amesema Gladness Stanford

Kamishna Hamdani Shemzigwa anahitimisha kwa kutoa rai kwa wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao katika chama hicho ili wafundishwe uzalendo wa kweli kwa taifa lao.

“Nawaomba wazazi wawalete watoto katika chama hiki ambazo ni jiko zuri la kuwalea watoto. Tunaamini kwamba inapokuwa na watoto 10 wa SKAUTI zaidi ya nusu watakuwa wazalendo na wataioenda nchi yao.” Amesema Kamishna Shemzigwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *