
Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji amesema Serikali imeondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika mafuta yaliyosafishwa yanayozalishwa na viwanda vya ndani kwa lengo la kupunguza bei ya mafuta ya kula ili yaweze kushindana na mafuta yanayotoka nje ya nchi.
Dkt. Kijaji ameyasema hayo leo Mei 21,2024 Bungeni Jijini Dodoma na wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Vile vile, katika mwaka 2022 Serikali ilifanya Mabadiliko ya Sheria ya Ushuru wa Forodha na kupunguza ushuru wa uagizaji wa mafuta ghafi ya chikichi (Crude Palm Oil) kutoka 25% hadi 0% ambapo lengo la mapendekezo hayo lilikuwa ni kusaidia viwanda vya ndani vinavyochakata mafuta ya chikichi (Crude Palm Oil) vipate malighafi na kusaidia upatikanaji wa bidhaa hiyo kwa bei nafuu”,amesema.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri kwa uwekezaji na hilo kupelekea kuongezeka kwa Mikoa inayolima mbegu za mafuta ya kula nchini kutoka mikoa 15 hadi mikoa 19 ambo hali hiyo inatokana na uhamasishaji wa programu ya kujitosheleza kwa mafuta ya kula nchini huku mikoa yenye uwezo wa kulima mbegu za mafuta imehamasishwa na kuanza kilimo hicho.