MSALALA WAJADILI MBINU KULETA MATOKEO CHANYA UFAULU WA WANAFUNZI


Mbunge wa jimbo Msalala, Alhaj Idd Kassimu Idd kwa kushirikiana na Umoja wa Walimu wakuu wa Shule za Sekondari wameanza mikakati ya kuinua ufaulu katika jimbo hilo, kwa kudhibiti utoro na kuongeza upatikanaji wa Chakula mashuleni.

Mikakati hiyo, inakuja siku chache baada ya kufanyika kikao kazi cha kutathmini hali ya Elimu kwa Mkoa wa Shinyanga kwa miaka mitano,
kilichoshirikisha Halmashauri ya Msalala, Ushetu na Manispaa ya Kahama kwa
awamu ya kwanza.

Wakiongea katika kikao hicho kilichofanyika katika kata ya Bulyankulu, Walimu hao wamesema moja kati mikakati yao ni kuimarisha upatikanaji wa chakula mashuleni kwakuwa wanafunzi wengi hawahudhurii masomo kwa kukosa chakula muda wa Masomo.

Mkuu wa Shule ya Mwl. Nyerere Sekondari, Kafulu Songola alisema, “suala la utoro msalala linaathiri sana maendeleo ya wanafunzi,Wanafunzi wanapokuwa hawapo shuleni Walimu wanaendelea na masomo sasa mwanafunzi siku anapokuja anakuta wenzake wamesoma mambo mengi na wengine wanakuja siku ya mtihani wa mwisho matokeo yake hawafanyi vizuri matokeo yao.”

Aidha, wameweka pia mkakati wa kuwashirikisha watendaji wa viviji na Kata Pamoja na wazazi katika kudhibiti utoro kwani wazazi wengi wanawatumia Wanafunzi kufanya kazi za nyumbani kama vile Kulima, Kuchunga na kufanya biashara ndogondogo katika minada mbalimbali siku ya soko.

“tuzidi kutoa elimu kwa wazazi,wapo baadhi ya wazazi wapo radhi kuwazuia Watoto wao wasiende shule ili wafanye shughuli za kiuchumi zikiwemo kufanya biashara hata wengine kufanya vibarua vya kulima ili familia zipate fedha,” aliongezea Mkuu wa Shule ya Bulige Sekondari, Mwl. Masonga Shauri.

Kuhusu wanafunzi wa kike wanaopewa ujauzito wamesema wataanzisha Klabu za maadili ambazo zinafundisha stadi za maisha na kuepuka vishawishi na walimu wa biologia wanafundisha elimu ya afya ya uzazi kwa kina na jinsi binti anavyoweza kujilinda ili kufikia ndoto zao.

“ Tumeanzisha klabu za maadili kule tunafundisha maadili na elimu ya
malezi, lakini pia Walimu wa biologia wanafundisha kwa kina elimu ya afya ya
Uzazi na tunafanya vikao vya shule Pamoja na jamii inayotuzunguka
tukihamasisha ushiriki katika malezi,” alisema Mwalimu Ikamaja Mazigwa, Mkuu wa Shule ya Sekondari Buyange.

Kufuatia maazimio hayo, Mbunge wa Jimbo la Msalala, Alhaj Idd Kassimu Iddy
amewapongeza wakuu wa shule kwa niaba ya walimu wote kwa juhudi kubwa za kufundisha wanafunzi Pamoja na kusimamia Ujenzi wa miundo mbinu ya Shule kwa uaminifu.

”Nawapongeza sana walimu, licha ya kufundisha mmeweza kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa Shule na mabweni tuliyoletewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, sijaenda hata sehemu moja nikasikia lawama wala mapungufu yoyote majengo haya hayana dosari kabisa ukiangalia ni majengo ambayo yamejengwa kwa ustadi na ubora mkubwa,” alisema.

Halmashauri ya Msalala ina jumla ya Shule za sekondari 26 na katika matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka 2024 halmashauri ya Msalala imekuwa ya pili kimkoa kati ya halmashauri sita za mkoa wa Shinyanga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *