Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Awamu ya pili ya kampeni ya msaada wa huduma ya kisheria inayofadhiliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayojulikana kama mama Samia Legal Aids kampeni na kutekelezwa na Wizara ya Katiba na Sheria inatarajiwa kuanza katika mkoa wa Shinyanga Mei 6 – 20, 2026 lengo likiwa ni kuwafikia asilimia hamsini ya wananchi wote wenye changamoto za kisheria.
Akizungumzia kampeni hiyo mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita amewataka wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kupata huduma hizo za kisheria huku akianisha namna kampeni hiyo kwa awamu ya kwanza ilivyowanufaisha wananchi.
Amesema katika awamu ya kwanza ya kampeni hiyo iliyofanyika mwaka 2023, jumla ya migogoro 578 ilishughulikiwa na kati yake migogoro 378 ilitatuliwa, huku zaidi ya wananchi 22,000 wakifikiwa na huduma hiyo.

RC Mhita amesema wananchi wa mkoa wa Shinyanga wanatarajiwa kunufaika na huduma za msaada wa kisheria bure kupitia kampeni hiyo , inayolenga kuwasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali za kisheria na kwamba timu ya watoa huduma za msaada wa kisheria itafika katika kata zote 130 za mkoa huo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
“Hii ni fursa muhimu kwa wananchi kwani huduma hizi zitawafikia moja kwa moja katika maeneo yao. Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata haki zao bila vikwazo vya kifedha. Rais Samia Suluhu Hassan tayari amelipia gharama zote za kampeni hii inayotekelezwa nchi nzima,” amesema RC Mhita.

Kwa mujibu wa Mhita, kampeni ya mwaka huu itaendeshwa kwa kipindi cha wiki mbili na itahusisha huduma mbalimbali zikiwemo ushauri wa kisheria, elimu kwa umma, uandaaji wa nyaraka za kisheria pamoja na uwakilishi katika vyombo vya mahakama.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kisheria Mkoa wa Shinyanga, John Shija, amesema wana matarajio makubwa katika awamu hii ya pili, akisisitiza kuwa kampeni hiyo itawafikia wananchi wa makundi yote na kusaidia kupunguza migogoro katika jamii.

Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo muhimu ili kupata msaada wa kisheria na kutatua changamoto zinazowakabili kwa njia halali na endelevu.
Naye mkurugenzi msaidizi wa uzingatiwaji wa huduma ya msaada wa kisheria Osborn Paissi ameielezea jambo media namna walivyojipanga kutekeleza zoezi hilo kwa weledi likilenga kuwafikia wananchi wote wenye matatizo ya msaada wa kisheria
Amesema katika awamu ya kwanza ya kampeni hiyo iliyotekelezwa mwaka 2023 migogoro ya aridhi iliongoza miongoni mwa changamoto za kisheria zilizowasilishwa katika kamati hiyo na kwamba wamejiandaa kuratibu vema kama wizara ya katiba na sheria ili kupunguza au kumaliza kabisa migogoro hiyo kisheria