MRUTU APETA KURA ZA MAONI CCM UBUNGE TABORA MJINI

Na Pascal Tuliano – Tabora.

Shabani Mrutu ameibuka mshindi katika kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Tabora Mjini baada ya kupata kura 6,612, hatua inayomweka katika nafasi nzuri ya kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Matokeo ya kura hizo yametangazwa rasmi usiku wa tarehe 4 Agosti 2025 na Katibu wa CCM Wilaya ya Tabora, Daniel Mhina, ambaye alieleza kuwa jumla ya kura zilizopigwa katika mchakato huo ni 7,882. Kati ya hizo, kura halali zilikuwa 7,763 huku kura 119 zikiripotiwa kuwa zimeharibika. Mhina amesisitiza kuwa zoezi hilo limeendeshwa kwa uwazi na amani, bila vurugu wala malalamiko makubwa kutoka kwa wagombea au wapiga kura.

Katika kinyang’anyiro hicho chenye ushindani wa watu sita, Mrutu amewaacha mbali wapinzani wake ambapo aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Emmanuel Mwakasaka, amepata kura 228 tu, huku Hawa Mwaifunga akikusanya kura 326. Kisamba Salehe Tambwe akipata kura 395, Deusdedith Kanunu kura 93, na Godbless Mafole kura 109.

Ushindi wa Mrutu unaelezwa na wachambuzi wa siasa za ndani ya chama kuwa ni matokeo ya juhudi zake za muda mrefu katika kujenga uhusiano wa karibu na wanachama, pamoja na kueleweka vyema kwa wapiga kura kwa sera zake. Aidha, baadhi ya wanachama waliohojiwa wameeleza kuwa Mrutu amekuwa mstari wa mbele katika masuala ya kijamii na maendeleo ya vijana, jambo lililompa nguvu kubwa katika mchakato huo.

Kwa matokeo haya, Shabani Mrutu sasa anasubiri uteuzi rasmi wa chama ili kuthibitishwa kuwa mgombea wa CCM kwa nafasi ya ubunge wa Jimbo la Tabora Mjini. Ikiwa atateuliwa, atakabiliana na wagombea kutoka vyama vingine katika Uchaguzi Mkuu ujao, ambapo macho ya wengi yataelekezwa Tabora Mjini kuona kama atafanikiwa kuendeleza ushindi huu hadi Bungeni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *