Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Serikali kupitia Wizara ya Nishati, imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa kitaifa wa umeme jua Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga, ambao ujenzi wake umefikia asilimia 78.5, ukigharimu Shilingi Bilioni 325.
Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo unaotarajiwa kukamilika Desemba 2025. Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema Serikali imeridhishwa na hatua zilizofikiwa, na kwamba kukamilika kwake kutasaidia kufikia malengo ya ajenda ya kimataifa ya nishati endelevu kwa wote ifikapo mwaka 2030.

“Tumefika kujionea utekelezaji wa mradi huu na kiukweli nimeridhishwa na kasi ya utekelezaji ambayo mkandarasi chini ya uongozi wa Dr Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma ya nishati safi, salama na nafuu. Kukamilika kwake kutaongeza upatikanaji wa umeme vijijini na kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati visivyo rafiki kwa mazingira,” amesema Mha. Mramba.
Kwa upande wake, Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Emmanuel Anderson amesema kasi ya ujenzi imeongezeka baada ya changamoto kadhaa zilizokuwa zikisababisha ucheleweshaji kutatuliwa na kwamba mkandarasi yuko katika hatua za mwisho za utekelezaji.

“Changamoto za awali kama ucheleweshaji wa vifaa na mvua nyingi sasa zimedhibitiwa. Mkandarasi anaendelea kwa kasi nzuri na matarajio yetu ni kuona mradi unakamilika kwa muda uliopangwa,” amesema Mhandisi Anderson.
Naye Meneja wa Kampuni ya Sinohydro inayotekeleza mradi huo, Injinia Daniel Xu, amesema kampuni yake imejipanga kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa ubora unaohitajika na ndani ya muda uliowekwa.

“Tumeongeza nguvu kazi na vifaa kuhakikisha tunamaliza kazi hii kwa wakati, tunathamini ushirikiano mzuri tunaoupata kutoka serikalini na wananchi wa Kishapu tunaahidi kukamilisha mradi huu kwa viwango bora,” amesema injinia Xu.
Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuongeza uwezo wa nchi katika kuzalisha umeme wa nishati jadidifu, kusaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa taasisi, viwanda, na wananchi, sambamba na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika mkoa wa Shinyanga.


