MRADI WA MAJI YA ZIWA VICTORIA KWENDA VIJIJI ZAIDI YA 30 WILAYA ZA SHY NA IRAMBA.

Na Gideon Gregory, Dodoma 

Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu wa awali kwa ajili ya Upanuzi wa Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria wa Tinde – Shelui kwenda zaidi ya vijiji 30 vya Wilaya za Shinyanga na Iramba. 

Waziri Aweso ameyasema hayo leo Aprili 24, 2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Dkt. Christina Mzava aliyehoji ni lini Serikali itapeleka Maji ya Ziwa Victoria katika Kata ya Usanda, Halmashauri ya Shinyanga.

“Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2025/26 na utafanyika kwa kipindi cha miezi 12,” amesema Aweso. 

Aweso ameongeza kuwa mradi huo utatekelezwa kwa utaratibu wa kusanifu na kujenga yaani (design and build) ambapo unatarajia kunufaisha wananchi 138,839 waishio kwenye Kata 12 za Wilaya za Iramba na Shinyanga ikiwemo Kata ya Usanda.

Aidha akijibu swali la nyongeza la Mbunge huyo juu ya lini wataanza kusambaza maji katika vijiji vinavyozungunga kata ya Tinde na Usanda, Waziri Aweso amesema kwasasa wapo katika hatua ya mwisho ya kumpata Mkandarasi atakayesambaza maji katika Vijiji vyote katika eneo la Tinde mpaka Didia.

“Nataka nikuhakikishie Mhe. Mbunge ili jambo tutalifanya kwasababu fedha zake zipo, lakini eneo la Nsalala Mhe. Spika katika awamu hii ya pili eneo hilo pia ni wanufaika katika kuhakikisha wanapata maji safi na salama,”amesema. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *