![](https://jambofm.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/2-59.jpg)
Na Gideon Gregory, Dodoma.
Ili kukabiliana na tatizo la maji katika Kijiji cha Kabulanzwili Mkoani Kigoma Serikali itakeleza ujenzi wa mradi wa maji unaotarajiwa kuanza mwezi Machi, 2025 na kukamilika ndani ya miezi tisa ili kuhudumia wananchi wapatao 14,138 wa vijiji vya Kabulanzwili na Chekenya.
Hayo yamebainishwa leo Februari 10, 2025 Bungeni hapa Jijini Dodoma na Waziri wa Maji Juma Aweso wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Josephine Gezambuke aliyetaka kujua ni lini Serikali itamaliza tatizo la upungufu wa maji katika kijiji cha Kabulanzwili – Kigoma.
“Serikali imeendelea kuboresha huduma ya majisafi na salama kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma ikiwemo kijiji cha Kabulanzwili kilichopo wilayani Kasulu mkoani humo,” amesema.
Amesema kuwa katika Mwaka wa Fedha 2024/25, Serikali inatekeleza mradi wa maji utakaohudumia vijiji viwili vya Kabulanzwili na Chekenya ambao upo katika hatua za mwisho za kusainiwa kwa mkataba.
“Kazi ya uchimbaji wa visima virefu viwili (2) ambavyo vitatumika kama vyanzo vya maji katika mradi huo imekamilika ambapo vina uwezo wa kuzalisha maji jumla ya lita 46,200 kwa saa,”amesema.
Waziri Aweso ameongeza kuwa kazi zingine zitakazo tekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa matanki mawili (2) yenye jumla ya ujazo wa lita 375,000, ulazaji wa mtandao wa mabomba umbali wa kilometa 36.6 sanjari na ujenzi wa vituo 29 vya kuchotea maji.