Na Ibrahim Rojala – Geita.
Ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Mwibuki kupitia Mradi wa Kuboresha Miundombinu ya Elimu ya Sekondari (SEQUIP) umeleta matumaini mapya kwa wakazi wa eneo hilo baada ya kupunguza adha ya wanafunzi waliokuwa wakitembea umbali wa takribani kilometa 16 kila siku kwenda na kurudi kufuata masomo.
Kabla ya mradi huo kutekelezwa, wanafunzi wa Mwibuki walilazimika kusafiri umbali mrefu kuelekea Shule ya Sekondari Ikunguigazi iliyopo Kijiji cha Kagera, hali iliyochangia uchovu, kuchelewa kufika shuleni na wakati mwingine kuwakatisha tamaa baadhi ya wanafunzi kuendelea na masomo.

Kutokana na changamoto hiyo, Serikali kupitia Mradi wa SEQUIP ilitoa shilingi 584,280,029 mnamo Septemba 2, 2024 kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Mwibuki, Ujenzi ulianza rasmi Januari 10, 2025 na kwa sasa umekamilika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela alipotembelea mradi huo hivi karibuni, Mkuu wa Shule hiyo, Veronicka Mboya Mradi alisema huo unajumuisha majengo 11 yaliyokamilika, yatakayowezesha wanafunzi kupata mazingira bora ya kujifunzia karibu na makazi yao na hivyo kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu kwa watoto wa kata hiyo na maeneo jirani.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa,mbali na uwekezaji wa Serikali, wananchi walitoa mchango mkubwa kwa kushiriki katika kazi mbalimbali za ujenzi ikiwemo kuchangia gharama za maji na kujaza vifusi kwenye majengo yote,mchango wao ukikadiriwa kuwa na thamani ya shilingi milioni 5.5, jambo linalodhihirisha ushirikiano mzuri kati ya Serikali na jamii katika kuboresha sekta ya elimu.

Shule mpya ya sekondari Mwibuki ambayo hivi sasa imekamilika na kupewa namba S.8511 na kuwa kituo cha mitihani namba S.7909. ina jumla ya wanafunzi 230 kati yao wasichana 124 na wavulana 106 ambo wote ni wananufaika wa sera ya elimu bure
Aidha kukamilika kwa Shule ya Sekondari Mwibuki kunatarajiwa kuongeza mahudhurio ya wanafunzi shuleni, kupunguza utoro unaotokana na umbali mrefu wa safari, kuboresha ufaulu wa wanafunzi na kuwapa wazazi nafuu ya gharama na muda waliokuwa wakitumia kuhakikisha watoto wao wanafika shuleni salama.

Mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha miundombinu ya elimu nchini kwa kusogeza huduma karibu na wananchi, kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kusoma katika mazingira salama, rafiki na yenye hadhi.
Utekelezwaji wa mradi huu umechangiwa na uamuzi wa serikali kutoa fedha kiasi cha bilioni 1.1 zilizoelekezwa katika elimu ya Sekondari ambazo kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbogwe, Wakili Edwin Bayona Lusa amesema zimetumika katika ujenzi wa vyumba vya madarasa, vyoo na ununuzi wa madawati.


