Na Daniel Gahu – Katavi.
Kikao Maalumu cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe kimefanyika kwa ajili ya kupitia Kitabu cha Hesabu za Mwisho za mwaka wa fedha 2025/2026, unaoishia Juni 30, 2026.
Kikao hicho, kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mpimbwe, kimewakutanisha madiwani, wataalamu wa halmashauri pamoja na viongozi mbalimbali kwa lengo la kujadili na kupitia taarifa za kifedha za halmashauri hiyo.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mlele, Yahaya Mburu, amewataka madiwani kuendelea kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zinazoongoza uendeshaji wa halmashauri ili kuhakikisha shughuli za serikali za mitaa zinafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji.
Mburu pia ameipongeza Halmashauri ya Mpimbwe kwa kutimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu muhimu ya maendeleo ya halmashauri hiyo.

Aidha, amesema taratibu zinaendelea kukamilishwa ili kuhakikisha watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wanapatikana katika Halmashauri ya Mpimbwe kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi, kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma hiyo.
Katika hatua nyingine, Katibu Tawala huyo amewataka viongozi na wananchi kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño, huku akisisitiza umuhimu wa kamati za maafa kuwa tayari wakati wote.

Amesema maandalizi hayo ni muhimu ili kuhakikisha hatua za haraka zinachukuliwa endapo kutatokea changamoto zinazoweza kuhatarisha maisha, mali na shughuli za wananchi.
Mburu pia amesisitiza umuhimu wa kukamilisha miradi ya maendeleo kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa, akieleza kuwa zimebaki siku 27 kabla ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru.

Kwa mujibu wake, miradi yote inayotarajiwa kutembelewa wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru inapaswa kuwa imekamilika na kuwa katika hali nzuri ili kuonesha matumizi sahihi ya rasilimali na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi.
Akizungumzia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Mburu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uhakiki wa Mikopo hiyo, amesema kuanzia Jumatatu ijayo wataanza ufuatiliaji wa mikopo chechefu.

Amesema zoezi hilo litafanyika kwa kushirikiana na Ofisi ya OCD pamoja na wataalamu wa halmashauri, kwa lengo la kuhakikisha fedha za mikopo zinarejeshwa ili kuwawezesha wananchi wengine wenye sifa kunufaika na mikopo hiyo.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa watumishi wanaohama vituo vya kazi kulipwa stahiki zao kwa wakati, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza malalamiko na changamoto zisizo za lazima miongoni mwa watumishi.

Akihitimisha kikao hicho, Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpimbwe, Method Kafwamagulu, amewakumbusha madiwani kuwa wao ni watumishi wa umma na hivyo wanapaswa kuwa sehemu ya kutafuta na kutoa majibu ya changamoto zinazowakabili wananchi.
Kafwamagulu amewataka madiwani kutokubaki katika nafasi ya kulalamikia changamoto, bali kutumia nafasi zao za uongozi kushirikiana na wataalamu pamoja na wananchi katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazojitokeza katika maeneo yao.
Amesema ushirikiano, uwajibikaji na kujikita katika kutafuta suluhisho ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maendeleo yanayokusudiwa.



