Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Phillip Mpango, ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kuhakikisha ununuzi wa umma unafanyika kupitia mfumo wa kielektroniki – NeST, ili kudhibiti vitendo vinavyosababisha ubadhirifu na upotevu wa fedha za umma.
Dkt. Mpango alitoa maelekezo hayo Februari 11, 2025, alipotembelea banda la PPRA kabla ya kufungua Mkutano wa Tano wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), Februari 11 – 13, 2025.
Akizungumza baada ya kusikiliza maelezo ya Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba, kuhusu ufanisi wa Mfumo wa NeST ulioanza kutumika Julai 1, 2023, Makamu wa Rais alisema anaamini matumizi ya mifumo thabiti ya kielektroniki yanaweza kuwa suluhu ya kudhibiti ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya watu, aliowafananisha na ‘mchwa’.
![](https://jambofm.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/IMG-20250212-WA0025-1024x682.jpg)
“Rai yangu, nikiangalia zile Ripoti za [ukaguzi] za PPRA, sipendezwi sana. Na mimi naamini kwamba mifumo thabiti ya kimtandao itatusaidia kudhibiti wale mchwa wanaotuharibiwa kwenye ununuzi. Unajua kuwa fedha kubwa ya umma, karibu asilimia 80, ni ununuzi.
Kwahiyo, nategemea PPRA mtusaidie kupunguza au kuondokana kabisa na hayo matatizo,” alisema Makamu wa Rais.
“Nadhani ninyi wataalam wa IT (TEHAMA), PPRA, chukueni ile Ripoti moja kwa mfano ya mwaka jana, halafu ainiesheni yale matatizo makubwa ni ya aina gani. Na je, mifumo inatusaidiaje kupambana nayo?” Dkt. Mpango aliongeza.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa PPRA alieleza kuwa Mamlaka hiyo imeanza kutekeleza maelekezo hayo kwa kuweka vizuizi vya ki-TEHAMA kwenye Mfumo wa NeST ili kukabiliana na udanganyifu na ubadhirifu unaoonekana kwenye Ripoti za Ukaguzi, kwa lengo la kuokoa fedha za umma na kupunguza hoja za ukaguzi.
![](https://jambofm.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/IMG-20250212-WA0024-1024x858.jpg)
Tumeanza kufanya hivyo Rais, na tumeona matokeo. Kwakuwa kwenye Mfumo wa NeST tumeweka mageti ambayo yanazuia wahalifu wasiweze kupita [na wakipita watambulike.
Kwa mfano, tatizo la mkataba kutoka bila kusainiwa na Bodi ya Zabuni, hiyo kwenye Mfumo wa NeST tumefunga, mkataba lazima usainiwe na Bodi ya Zabuni, na ripoti ya Kamati ya Tathmini lazima isainiwe na wajumbe husika,” alisema Simba.
![](https://jambofm.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/IMG-20250212-WA0026-1024x678.jpg)
Aidha, Simba alitaja changamoto kubwa inayojitokeza hivi sasa kuwa ni uelewa na elimu kwa umma, ambapo Mamlaka hiyo imeendelea na jitihada za kutoa elimu kwa wadau, ikiwa ni pamoja na kutumia njia za mtandao ili kuongeza kasi ya kuwafikia.
Baada ya kusikiliza maelezo kuhusu Mfumo wa NeST, Makamu wa Rais aliipongeza PPRA kwa hatua iliyofikiwa, ambapo hadi sasa, mikataba yenye thamani ya takribani Shilingi Trilioni 14 imekwishatolewa kupitia Mfumo wa NeST tangu ulipoanzishwa.