MOTO WAHARIBU ZAIDI YA HEKTA 705 ZA MISITU YA HIFADHI MISSENYI, CHANZO CHATAJWA

Na Cecilia Shiratu, Missenyi – Kagera.

Matukio ya moto katika Misitu ya Hifadhi Wilayani Missenyi mkoani Kagera, yameendelea kuongezeka, ambapo katika kipindi cha miezi miwili zaidi ya matukio nane ya moto yameripotiwa katika misitu ya Minziro, Ruhasina na Kikuru, yakiharibu zaidi ya hekta 705 za misitu inayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Mhifadhi wa Misitu Wilaya ya Missenyi, Mrisho Athumani, amesema matukio hayo yametokana kwa kiasi kikubwa na shughuli za kibinadamu zinazofanywa na baadhi ya wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi.

Amesema, ipo haja kwa Wananchi kubadilika na kuwa na mtazamo chanya kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa rasilimali za misitu, ili kuhakikisha misitu hiyo inalindwa na kizazi cha sasa pamoja na vizazi vijavyo.

“Wananchi wanapaswa kutambua kuwa misitu ni rasilimali muhimu katika maisha yetu, hivyo tunahitaji kushirikiana kuilinda dhidi ya matukio ya moto ambayo yanaendelea kusababisha uharibifu mkubwa,” amesema Athumani.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali Mstaafu Hamisi Maiga, alitembelea eneo lililoathiriwa na moto na kuwataka watendaji wa vijiji na kata kuchukua hatua za haraka katika kudhibiti na kuzuia matukio ya moto.

Amesisitiza umuhimu wa viongozi wa maeneo husika kushirikiana na wananchi katika kutoa elimu na kuchukua tahadhari zinazohitajika, ikiwemo kudhibiti shughuli zinazoweza kusababisha moto katika maeneo ya misitu ya hifadhi.

Kwa upande wao baadhi ya Wananchi walieleza namna wanavyoathirika kutokana na matukio ya moto katika maeneo hayo, sambamba na hofu yao kuhusu hatari ya kupotea kwa misitu hiyo endapo hatua madhubuti za kudhibiti moto hazitachukuliwa.

Serikali na wadau wa uhifadhi wametakiwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza misitu na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na moto.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *