Na Gideon Gregory – Dodoma.
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeongeza matumizi ya Akili Unde (AI) katika huduma za upasuaji, hususan upasuaji wa mfumo wa fahamu, hatua inayolenga kuongeza usahihi na ufanisi wa matibabu.
Mkurugenzi wa MOI balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, ameyasema hayo leo Septemba 1, 2026, jijini Dodoma, wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2025/2026 na mwelekeo wa mwaka 2026/2027.

Amesema matumizi ya AI yameimarika baada ya taasisi hiyo kuongeza mitambo na wataalamu wenye uwezo wa kutumia teknolojia hiyo, hivyo kuwezesha utoaji wa huduma kwa ufanisi zaidi.
Kwa mujibu wa Dkt. Ulisubisya, vipimo vya mgonjwa vinapochukuliwa huingizwa kwenye mfumo wa AI unaochakata taarifa na kutengeneza ramani inayomsaidia daktari kubaini kwa usahihi eneo lenye tatizo kabla na wakati wa upasuaji.
Amesema teknolojia hiyo humwezesha daktari kulenga eneo lenye tatizo kwa usahihi zaidi, jambo linalosaidia kuongeza uhakika na ufanisi wa upasuaji.
Aidha, Dkt. Ulisubisya amesema matumizi ya AI yamewawezesha wataalamu wa MOI kuchukua sampuli za wagonjwa na kuziwasilisha kwa uchunguzi wa maabara kwa usahihi na ufanisi zaidi.


