MNEC HAMOOD AWAPA SOMO WANANCHI UMUHIMU WA UCHAGUZI MKUU

MNEC Hamood Abuu Jumaa awaongoza Wananchi Mlandizi kujitokeza kujiandikisha kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya (CCM) Taifa kupitia Jumuiya ya Wazazi, Hamood Abuu Jumaa, ameongoza kampeni ya uhamasishaji kwa wananchi wa Mlandizi kujitokeza kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ikiwa ni maandalizi ya kushiriki Uchaguzi Mkuu ujao.

Akizungumza mbele ya mamia ya wakazi wa eneo hilo, Hamood leo Jumatano Mei 22,2025 amesisitiza kuwa kila mwananchi mwenye sifa ya kupiga kura anapaswa kuchukua hatua ya kujiandikisha ili kuweza kushiriki mchakato wa kuamua viongozi wa taifa.

“Ni muhimu kuelewa kuwa kutokujiandikisha kunamaanisha kupoteza haki yako ya msingi ya kuchagua viongozi. Ukomavu wa kidemokrasia huanza na hatua kama hii,” amesisitiza Hamood.

Aidha, amewakumbusha wanachama wa CCM kuwa na subira na kufanya kampeni za kistaarabu pindi muda wa kampeni utakapowadia kwakuwa chama Hi ho kinaheshimu sheria za nchi.

“Tujitofautishe kwa hoja, si kwa kejeli wala matusi. CCM ni chama cha watu wastaarabu na tunataka kuendeleza taswira hiyo,” ameongeza.

Hata hivyo kiongozi huyo amewakumbusha wakazi wa eneo hilo kutunza kumbukumbu juu ya maendeleo yanayotekelezwa na uongozi uliopo madarakani kuanzia ujenzi wa miundombinu na huduma za kijamii.

“Tunapaswa kutunza kumbukumbu tumetoka wapi tuko wapi na tunakwenda wapi ili muda wa kupiga kura ukifika tufanye uamuzi wa busara kwa kuchagua viongozi waliotuletea maendeleo”amesema

Wakazi wa Mlandizi wamepokea kwa shukrani wito huo, wakisema umeleta mwamko mpya.

Asha Mohamed, mkazi wa eneo hilo, amesema, “Hii ni hatua nzuri wengi wetu tulikuwa hatujui umuhimu wa zoezi hili lakini sasa tumehamasika.” amesema.

Naye Paulo Yohana ameongeza, “Tunampongeza kiongozi huyu kwa kutufikia moja kwa moja na tupo tayari kujiandikisha.”amesema

Kampeni hiyo inaendeshwa kwa kushirikiana na viongozi wa CCM wa ngazi ya Mkoa, ambapo tayari Hamood na timu yake wamefika Kisarawe na Bagamoyo, kabla ya kuhitimisha leo Mlandizi, Kibaha Vijijini, mkoani Pwani.

Zoezi la uandikishaji linaendelea katika mikoa mbalimbali nchini kwa ratiba ya Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), na wananchi wanahimizwa kufuatilia taarifa rasmi ili kujua siku na maeneo ya kujiandikisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *