
Na Gideon Gregory,Dodoma
Wizara ya Katiba na Sheria imekamilisha uandaaji wa muswada wa marekebisho ya Sheria ya Ndoa na ambapo kwa sasa muswada huo upo katika hatua za ndani za Serikali mara hatua hizo zitakapokamilika, muswada huo utawasilishwa Bungeni kwa utaratibu wa kawaida.
Hayo yameelezwa leo Mei 22,2024 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Jumanne Sagini wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Dkt. Thea Ntara aliyetaka kujua ni lini Serikali italeta Muswada wa Sheria ya Ndoa ili iendane sambamba na vita dhidi ya ndoa za utotoni.
“Mheshimiwa Spika, baada ya maamuzi ya Mahakama ya Tanzania, Serikali iliwasilisha bungeni muswada wa marekebisho ya Sheria ya Ndoa kupitia Tangazo Na 1. Vol 102 tarehe 5 Februari, 2021 kwa kupendekeza umri wa kuoa au kuolewa uwe miaka 18,”amesema.
Aidha, ameongeza kuwa Bunge kupitia Kamati ya Uongozi ilielekeza Serikali kukusanya maoni ya wananchi kuhusiana na suala hilo, baada ya maelekezo hayo, Serikali ilikusanya maoni ya wananchi, vilevile, tarehe 26 Aprili, 2023 Serikali ilifanya Kongamano la Sheria ya Ndoa Dodoma ili kupata maoni zaidi kuhusu umri wa kuingia kwenye ndoa.