Mgombea udiwani wa Kata ya Tangini, Jimbo la Kibaha Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mlao amewataka wananchi kudumisha amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Mailimoja B, Manispaa ya Kibaha, Mlao amesema Serikali imejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa utulivu, na kwamba hakuna sababu ya kuingiwa na hofu kutokana na uvumi wa maandamano.

Amesema Serikali imekuwa mstari wa mbele kulinda usalama wa wananchi na kuhakikisha kila mmoja anatekeleza haki yake ya kidemokrasia kwa amani.
Pamoja na hilo, Mlao ameahidi kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotengewa fedha ndani ya kata hiyo, ikiwemo ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 13 na soko la kisasa lenye thamani ya zaidi ya Sh 8 bilioni.

Amesema miradi hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha miundombinu na huduma za kijamii, na akaahidi kuhakikisha fedha hizo zinatumika ipasavyo ili wananchi wanufaike.
Baadhi ya wakazi wa kata hiyo, wamesema wanachokiomba zaidi ni amani kipindi chote cha uchaguzi, wakisisitiza kuwa bila utulivu hakuna maendeleo yatakayofanyika.

“Kikubwa ni amani na utulivu hilo ni jambo la msingi hivyo ni vema wananchi wakatulia na kufuata sheria”amesema Veronica Semwaiko
Anitha Mwaimu amesema uwepo wa amani ndiyo msingi wa maendeleo, kwani bila utulivu, hata miradi mikubwa haiwezi kufanikiwa.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unatarajiwa kufanyika nchini kote Oktoba 29, 2025.


