Kufuatia Tanzania kuwa Mwenyeji wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hali ya usalama imeimarishwa na baadhi ya barabara zitafungwa kwa muda na kufunguliwa ili kupisha misafara ya Viongozi wa mkutano huo.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Jumanne Muliro imeeleza kuwa barabara ambazo zitafungwa kwa muda na kufunguliwa ni Barabara ya Nyerere kutokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwenda katikati ya Jiji, Barabara ya Sokoine, Kivukoni na Lithuli kuanzia taa za Gerezani kwenda Hoteli ya Johari Rotana, Hyatt Regency hadi Ikulu.

Nyingine ni Barabara ya Ohio kutokea Kivukoni kwenda Hoteli ya Serena na Barabara ya Garden kutokea barabara ya Lithuli kwenda Hoteli ya Southern Sun.
Tayari hii leo Mawaziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wamekutana jijini Dar es Salaam, kujadili mzozo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC), ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kikao cha Marais wa jumuiya hizo, kitakachofanyika hapo kesho Februari 8, 2025.


