Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Tabora, Said Juma Nkumba, amefungua kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa kilichofanyika Agosti 12, 2026 wilayani Kaliua, akiwataka watumishi wa Serikali kuhakikisha ahadi zilizomo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025–2030 zinatekelezwa kikamilifu, ili wananchi wapate huduma bora.
Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Siasa, Katibu wa CCM Mkoa, Wilson Khambaku, amesema Kamati imekagua miradi 13 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 4.5 na kuridhishwa na ubora wake pamoja na thamani ya fedha iliyotumika.

Pia imehimiza miradi hiyo kulindwa na kuimarishwa kwa usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora, IGP (Mst.) Balozi Simon Sirro, amesema Serikali imetoa takribani shilingi bilioni 465 kwa miradi ya maendeleo mkoani Tabora katika kipindi cha Januari hadi Juni 2026.

Aidha, mapato ya ndani yameongezeka kwa asilimia 23, kutoka shilingi bilioni 40.21 hadi shilingi bilioni 49.46.
Katika kikao hicho, wajumbe wamejadili changamoto za bei, ubora na masoko ya tumbaku huku Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku Tanzania, Stanley Mnozya, ameahidi kuandaa mafunzo maalumu kwa wadau, huku Ndg. Nkumba akiwataka wakulima kuzalisha tumbaku inayokidhi viwango ili kulinda soko na kupata bei nzuri.

Kikao kijacho cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Tabora kinatarajiwa kufanyika mapema mwaka 2027 wilayani Sikonge.




