PATO LA MKOA WA SINGIDA LAONGEZEKA – RC DENDEGO.

Na Gideon Gregory, Dodoma 

Imeelezwa kuwa Pato la Mkoa wa Singida limeongezeka kutoka Trioni  2.709 mwaka 2020/21 hadi Trilioni 3.398 mwaka 2024/25 huku wastani wa pato la  mwananchi mmoja mmoja likiongezeka kutoka zaidi ya Milioni 1.588 mwaka 2020/21 hadi  zaidi ya Milioni 1.710 mwaka 2024/25.

Hayo yameelezwa leo Julai 4,2025 na Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego wakati akizungumza na waandishi wa habari hapa Jijini Dodoma wakati akibainisha mafanikio ya mkoa huo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Pato la Mkoa limeongezeka kutoka Tshs. 2.709 Trilioni mwaka 2020/21 hadi shilingi Trilioni 3.398 mwaka 2024/25, wastani wa pato la mwananchi mmoja mmoja umeongezeka kutoka Tshs. 1,588,604.66 (2020/21) hadi Tshs. 1,710,562.00 mwaka 2024/25.

Aidha amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imewezesha Mkoa wa Singida kupokea kiasi cha shilingi trilioni 1.72 kwa kipindi cha miaka mitano (2020–2025). 

Fedha hizo zimetumika kugharamia shughuli za uendeshaji wa Serikali na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, miundombinu, maji, kilimo na utawala bora.

“Kwa mwaka 2022/23, kiasi cha shilingi bilioni 239.81 kilitengwa, na shilingi bilioni 221.66 zilitolewa, sawa na asilimia 92 ya bajeti. Mwaka 2023/24, Serikali ilitoa shilingi bilioni 241.65 kati ya bilioni 230.99 zilizopangwa, sawa na asilimia 105,” amesema na kuongeza; Katika mwaka wa fedha wa mwisho wa kipindi hicho (2024/25), shilingi bilioni 236.29 zilitolewa kati ya bilioni 259.35 zilizotengwa, sawa na asilimia 91 ya bajeti“ amesema.

Amefafanua kuwa katika kipindi hicho hicho, Mkoa wa Singida umeongeza pato lake la ndani (Regional GDP) kutoka shilingi trilioni 2.709 mwaka 2020/21 hadi shilingi trilioni 3.398 mwaka 2024/25. Wastani wa pato la mwananchi mmoja mmoja umeongezeka kutoka shilingi 1,588,604 hadi shilingi 1,710,562.

“Mkusanyiko wa mapato kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) umeongezeka kwa kasi kutoka shilingi bilioni 11.9 mwaka 2021/22 hadi shilingi bilioni 30 mwaka 2024/25  sawa na ongezeko la asilimia 152,mapato ya ndani ya halmashauri za mkoa yameongezeka kutoka shilingi bilioni 14.6 hadi bilioni 24.8, ongezeko la asilimia 69.8,”amesema.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, mkoa una idadi ya wakazi 2,008,058 ambapo wanaume ni 995,703 na wanawake ni 1,012,355 huku zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa mkoa huo wanategemea kilimo na Ufugaji kama shughuli kuu za kiuchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *