Wilaya ya Nyang’hwale, mkoani Geita, imepanda jumla ya miti 926,944 katika mwaka wa fedha 2023/24. Hii ni asilimia 61.79 ya lengo la kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka ambapo mradi huo umetekelezwa kwa ushirikiano na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na wadau wengine wa mazingira.
Akitoa taarifa ya upandaji huo wa miti mbele ya kiongozi wa mbio za mwenge alipotembelea Shule ya Sekondari Igalula Mining afisa Misitu wilaya ya Nyang’hwale Mrema Juma amesema mradi huo ulianza Novemba 2023 na jumla ya miche 643 ilipandwa shuleni hapo kati yake kuna miti ya kivuli na ya matunda.
Mrema amesema Lengo kuu la mradi huo ni kuboresha mazingira ya shule, kusaidia afya ya wanafunzi kupitia kivuli na matunda, pamoja na kulinda majengo dhidi ya upepo mkali ambapo Miti hiyo imepandwa pia kwenye taasisi mbalimbali kama shule, zahanati, vituo vya afya na ofisi za umma.
Ameongeza kuwa halmashauri hiyo haikufikia lengo la kupanda miti milioni 1.5 mwaka huu kutokana na ucheleweshaji wa miche kukabiliana na changamoto hii na kwamba vitalu viwili vya miche vitaanzishwa kwa kutumia fedha za CSR na Forest Fund ili kusaidia kufikia lengo la mwaka 2024/25.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Godfrey Mzava, amesisitiza umuhimu wa kuendelea na juhudi za upandaji miti ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kampeni inayopaswa kuwa endelevu kwa ustawi wa mazingira na vizazi vijavyo.