Mwanaume mmoja aliefahamika kwa jina la Elia Mayoyo (51) Mkazi wa Mtaa wa Msalala Road Halmashauri ya Mji wa Geita Mkoani Geita amewashangaza wakazi wa mtaa huo baada ya kukutwa na rundo la taka na uchafu wa aina mbalimbali ndani ya chumba anacholala kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10 hali iliyoleta taharuki kwa wakazi wa mtaa huo.
Kwa mujibu wa majirani na wamiliki wa nyumba anayoishi mwanaume huyo wamesema amekaa kwa muda wa zaidi ya miaka kumi katika chumba hicho akikusanya taka kila kukicha na kuziweka ndani na alipotakiwa kuondoka aligoma hali iliyopelekea kutolewa kwa amri ya mahakama na ndipo akakubali kuhama na kuanza kutoa mizigo yake nje zikiwemo taka na uchafu huo.
Akizungumza na Jambo Fm Elia Mayoyo amesema taka hizo zilizokutwa ndani ya chumba hicho ikiwemo kinyesi cha popo pamoja uchafu mwingine amevikusanya kwa zaidi ya miaka 10 kwa lengo la kuzibadilisha kuwa mbolea ya asili ili aweze kuuza kwa lengo la kujipatia kipato.