Na Daniel Gahu – Katavi.
Kwa kutambua umuhimu huo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, ameshiriki zoezi la upandaji miti katika Shule ya Msingi Songambele, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mlele, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa maadhimisho ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza mara baada ya zoezi hilo, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kiongozi mwenye maono makubwa, ambaye katika kipindi kifupi cha uongozi wake amefanya kazi kubwa ya kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu, huduma za jamii na uhifadhi wa mazingira katika Mkoa wa Katavi.

Ameeleza kuwa zoezi la upandaji miti halipaswi kuishia katika kugawa miche pekee, bali waliopokea miche hiyo wana wajibu wa kuhakikisha wanaipanda na kuisimamia ipasavyo hadi ikue. “Kupanda mti ni hatua ya kwanza, lakini kuutunza hadi ukue ndio dhamira halisi ya zoezi hili,” amesisitiza RC Mrindoko.
Aidha, amesema maelekezo ya Serikali ni kuhakikisha kila Halmashauri inapanda angalau miti milioni 1.5, na ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mlele kwa juhudi zake kubwa katika utekelezaji wa mpango wa upandaji miti. Hata hivyo, amezitaka Halmashauri zote za Mkoa wa Katavi kuongeza kasi na kuendelea na zoezi hilo kabla ya msimu wa mvua haujatamatika.

Katika hatua nyingine, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mlele kusimamia kwa ukaribu suala la watoto wote kuripoti na kuhudhuria shule ipasavyo, akisisitiza kuwa elimu ni msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Amehimiza wazazi na walezi kushirikiana na viongozi kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nje ya mfumo wa elimu.

Zoezi hilo limehudhuriwa na viongozi wa Serikali, watendaji wa Halmashauri, walimu, wanafunzi pamoja na wananchi wa eneo la Songambele, likiwa na lengo la kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya elimu.


