MITI 500 YAPANDWA SHINYANGA KUADHIMISHA SIKU YA KUZALIWA YA RAIS SAMIA.

NA EUNICE KANUMBA –SHINYANGA 

Serikali mkoani Shinyanga imeadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupanda miti 500 katika Shule ya Msingi Mapinduzi, iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga. 

Tukio hili limefanyika leo, Januari 27, 2025, ikiwa ni siku ya kuzaliwa kwa Rais Samia, ambaye alizaliwa  tarehe na mwezi kama wa leo mwaka 1960, na hivyo kufikisha umri wa miaka 65.

Katika kuendeleza jitihada za serikali za utunzaji wa mazingira, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha, ameongoza kampeni hii ya upandaji miti. 

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Macha amesema kwamba mkoa wa Shinyanga umeamua kupanda miti 500 katika shule hiyo kama sehemu ya kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa Rais Samia, lakini pia ni sehemu ya kutekeleza maelekezo yake kuhusu utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Miti hii 500 tumeipanda leo, siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kupanda miti ni heshima kubwa kwa Rais wetu na ni moja ya hatua muhimu katika kuhakikisha mazingira yetu yanatunzwa. Naagiza miti hii itunzwe na ikue vizuri, ili siku tukija hapa tuone mazingira yanavyokuwa,” amesema Macha.

Aidha, Macha amesisitiza kuwa wananchi, taasisi na halmashauri za mkoa wa Shinyanga wanapaswa kuendelea na kampeni ya kupanda miti katika maeneo yao.

RC Macha pia  Amewataka wafugaji na wananchi wanaochunga mifugo katika maeneo yaliyopandwa miti kuchukuliwa hatua kali ikiwa watabainika kuvunja sheria za utunzaji wa mazingira. 

Amesema ,“Mti mmoja ukikatwa, ipandwe miti zaidi ya miwili,” na kuonya dhidi ya tabia ya kukata miti kiholela bila kibali cha mamlaka husika.

Katika hatua nyingine, Macha ametoa pongezi kwa Rais Samia kutokana na utendaji wake mzuri, akitolea mfano Mkutano Mkuu wa Masuala ya Nishati uliofanyika Tanzania na kuwakutanisha viongozi kutoka nchi mbalimbali. 

Amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni muhimu, kwani yanaweza kupunguza utegemezi wa mkaa, ambao unachangia uharibifu mkubwa wa mazingira.

 Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, ameonyesha dhamira ya kuendeleza kampeni ya kupanda miti, huku akihakikisha kuwa miti 500 iliyopandwa itafuatiliwa na itatunzwa. 

Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Elias Masumbuko, ameeleza kuwa maelekezo yote aliyotoa Mkuu wa Mkoa yatatekelezwa, na pia wataendelea kuhamasisha wananchi na halmashauri kujiunga na kampeni hii ya kupanda miti.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mapinduzi, ambao wamehusika katika zoezi la kupanda miti, wameonesha furaha yao na kuelezea umuhimu wa kupanda miti. 

Mwanafunzi Godfrey Mgeta ameelezea jinsi walivyofahamu umuhimu wa miti,na ameahidi kuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha familia zao na jamii kuendelea kupanda miti katika maeneo yao.

Zoezi hili limemalizika kwa kumuimbia Rais Samia wimbo wa “Happy Birthday,” kama ishara ya heshima na upendo kutoka kwa wananchi wa Shinyanga.

Sherehe za kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkoa wa Shinyanga ni mfano mzuri wa jinsi jamii inavyoshirikiana na serikali katika kudumisha mazingira bora na kuhamasisha utunzaji wa rasilimali za taifa.

 Kupanda miti si tu ni hatua ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, bali pia ni ishara ya uzalendo na dhamira ya dhati ya kuendelea kulinda dunia yetu kwa vizazi vijavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *