
Mkazi wa Mtaa wa Majengo Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga Rajabu Msimbe ambaye ni Mfanyabiashara wa Vyuma Chakavu anashilikiwa na Jeshi la Polisi mkoa Shinyanga kwa tuhuma ya kukamatwa na Dira mbili za Maji Mali ya Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA) zilizokuwa zimefungashwa kama vyuma chakavu.

Hayo yamejiri katika mtaa wa Mhongolo ambapo jeshi la polisi lilifika na maafisa wa Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA) na kufanya upekuzi katika eneo hilo baada ya kupata taarifa za siri kutoka kwa wasamalia wema.
Akizungumza na waandishi wa Habari Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA) John Mkama amesema kuwa kuanza mwezi octoba mwaka jana hadi leo April 23 mita za maji 210 zimeibiwa maeneo tofauti ya manispaa ya Kahama na kusababisha hasara ya Shilingi Milioni 25.2.

“Changamoto hii imeeanza tangu Octoba 2024 na tangu kipindi hicho jumla ya dira 210 zimeibiwa ambazo kila dira moja ni shilingi laki moja na ishirini sasa kwa dira hizi ambazo zimeibiwa zina jumla ya shilingi milioni 25 na laki mbili” Amesema Mkama.

Sambamba na hayo Mkama amesema kuwa kwakuwa wamemkamata mtuhumiwa huyo sasa watajua dira hizi zinaenda kufanya kazi gani,zinaenda wapi na soko lake liko wapi.
“Kwakuwa leo tumemkamata huyu mmoja ambaye anahusika na kununua dira hizi,yeye atatwambia dira hizi wanazipeleka wapi na soko liko wapi akishabanwa na vyombo husika atasema na sisi tutakuja kwa umma kuwaeleza wapi zinapopelekwa dira hizi” Ameongeza Mkama.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Mhongolo Charles Nangale ameshuhudia tukio hili na kutoa wito kwa wanunuaji wa vyuma chakavu katika mtaa wake kuacha kununua nyara za serikali na kuwataka wananchi wanaofanya wizi huo kuacha kuharibu miundo mbinu hiyo.
“Kuna vifaa vya mamlaka ya Maji vimekamatwa katika mtaa wangu,na matukio ya wizi wa mita yamekuwa mengi sana Manispaa ya Kahama hivyo niwaombe wanaofanya biashara ya vyuma chakavu katika mtaa wangu waache kununua nyara za serikali na wale wanaioba vifaa hivi waache tabia hii mana serikali ipo na msako unaendelea” Amesema Nangale.
Awali akieleza namna alivyozipata dira hizo Mfanyabiashara wa Vyuma Chakavu Rajabu Msimbe amesema kuwa katika ofisi yake hawana utaratibu wa kununua dira hizo na wakati zinanunuliwa hakuwepo eneo hilo.
“Hivi vifaa vimenunuliwa mimi sikuwepo na wakati wanasema wakague nilijiamini sana mana hatuna utaratibu wa kununua mita za maji sasa huyu kijana alipoyanunua aliacha kuyamwaga akaweka tu na mfuko kumbe yamo humo” Amesema Rajabu.
Nao baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Kahama Shakira Mohamedi na Sharifu Katala wamesema kuwa zinapoibiwa dira za maji gharama ya kurejesha huduma ni kubwa na kwamba hatua zichukuliwe kwa wahusika na wanaonunua vyuma chakavu watoe taarifa pindi wanapoletewa vifaa vya serikali.
“Wafatiliwe watajane ili iwe fundisho mana vikiibiwa gharama kubwa kurejesha huduma, Kiukweli siyo sawa wanavyofanya na tuwaombe wanaonunua vyuma chakavu watoe taarifa pindi wanapoletewa vifaa vya serikali kama hizi mita na hata Nyaya na vifaa vingine vya Tanesco” Wamesema wakazi hao.


