Na Clavery Christian – Kagera
Mbunge wa Jimbo la Missenyi, Florenti Laurent Kyombo, ameweka wazi kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake, miradi ya maendeleo jimboni humo imetekelezwa kwa kiwango cha asilimia 93.5, hatua ambayo imeleta mabadiliko makubwa katika nyanja mbalimbali za huduma kwa wananchi.
Akizungumza katika kilele fainali ligi ya Dokta Samia na Kyombo CUP aliyoianzisha mbunge Kyombo iliohudhuriwa na viongozi wa serikali na wananchi, alisema kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano wa karibu kati yake, wananchi na serikali.
“Tumejenga shule, vituo vya afya, barabara na kusaidia vifaa vya usafiri kwa maeneo ya mwambao. Katika sekta ya miundombinu, tumeweza kununua boti na mitumbwi kwa ajili ya kusaidia usafiri kwa wananchi wa maeneo ya Rushenye na Busheregenya.,” alisema Mbunge Kyombo.

Amesema kuwa wameweza kusimamia ipasavyo miradi ya maji, umeme, elimu na afya kwa kuhakikisha kila kijiji kinafikiwa na huduma za msingi, sambamba na kusukuma mbele ajenda ya maendeleo jumuishi.
Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali Mstaafu Khamis Maiga, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Kagera Hajjat Fatma Mwassa akiwa mgeni Rasmi katika fainali hiy amepongeza juhudi za Mbunge Kyombo kwa kusema kuwa, mchango wake umesaidia kuimarisha mapato ya halmashauri, hali iliyowezesha kutekeleza miradi mingi ya kijamii.
“Mbunge amekuwa kiungo muhimu katika mafanikio ya Missenyi. Tumeshuhudia ongezeko la mapato ya halmashauri, na elimu katika wilaya imepanda kwa kiwango cha kuridhisha kitaifa,” alisema Kanali Maiga.

Wananchi wa Missenyi wameendelea kuonyesha imani yao kwa Mbunge Kyombo wakisema kuwa, uongozi wake umeleta mabadiliko makubwa, na wana matumaini makubwa kwa awamu ijayo ya maendeleo.
Katika Fainali hiyo Timu ya Kassambya iliibuka kifua mbele kwa ushindi wa penati 7 – 6 baada ya mchezo huo kumalizika kwa kufungana goli 1 – 1 timu ya Kashenye na mshindi wa mchezo huo ameondoka na shilingi milioni 3 na kombe huku mshindi wa pili akiondoa na shilingi milioni 2 taslimu.