Na Afarah Suleiman, Simanjiro – Manyara.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Joseph Ole Milya amewapongeza wawekezaji kutoka China waliowekeza kwa ubia na Watanzania kwenye kiwanda cha kuchakata madini ya kinywe (GRAPHITE), yanayotumika kutengeneza Betri za Magari yanayotumia umeme na bidhaa za kielektroniki.
Amesema, hatua hiyo inasaidia kuongeza mapato ya Wilaya ya Simanjiro na Tanzania kwa ujumla, pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa vijana wa Kitanzania.

Akizungumza katika uzinduzi wa Kiwanda hicho cha kuchakata Madini ya Graphite, ikiwa ni uwekezaji wa shilingi Bilioni 50 wa Kampuni ya Parmanent Minerals katika Kijiji cha Kandasikira Kata ya ShambaLai, Milya amepongeza ushiriki wa China kwa uwezekezaji wake hapa nchini.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Permanent Minerals Company amesema, kiwanda hicho kinazalisha takribani tani 6000 kila mwezi na kuziuza katika mataifa mbali mbali ikiwemo China, Marekani na India, huku Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa aliyezindua mradi huo akitoa pongezi kwa Wawekezaji.

Katika hatua nyingine, mbio za Mwenge wa Uhuru zimeweka jiwe la msingi katika Wodi ya Wanawake Kituo cha Afya cha Mirerani, iliyojengwa na wadau maendeleo wa Kampuni ya Chusa Mining.
Ukiwa Mkoani Manyara, Mwenge wa Uhuru unatarajia kuzindua, kuweka mawe ya Msingi na kutembelea jumla ya miradi ya maendeleo 49 yenye thamani ya Bilioni 139,926 901,532.42 ambapo utakimbizwa kilometa 1371.70.







