Na Adam Msafiri, Tarime – Mara.
Jeshi la Polisi nchini limesema mila potofu na zilizopitwa na wakati kama vile vitendo vya ukeketaji, hazikubaliki katika jamii ya sasa na kwamba wataendelea kuchukua hatua kwa kuwakamata wale wote wanaoendeleza mila za namna hiyo zenye madhara kwa ustawi wa jamii.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Kamanda Camilius Wambura Juni 24,2025 akiwa wilayani Tarime mkoani Mkoani Mara ambapo amesema”Mila hizi zenye madhara kwa watoto wa kike hazina nafasi katika jamii ya leo sisi kama Jeshi la Polisi tumeazimia kupambana na mambo hayo kisheria,kielimu na kijamii hadi mila hizo zifutike kabisa’’.

Aidha Kamanda Wambura ameeleza kwamba”Wataendelea kubaini wahusika,kuwaleta wahanga na kujitokeza mbele kupinga mila hizo zilizopitwa na wakati pamoja na kuisisitiza jamii wanawake na wanaume kutambua kuwa mapambano dhidi ya vitendo hivyo vya ukatili ni ya pamoja”.
Naye kamanda wa Polisi kanda maalumu ya kipolisi ya Tarime-Rorya Mark Njera amesema kuwa kwa kiasi kikubwa wananchi kwa sasa wameelimika na wameecha kufumbia macho matukio na vitendo vyenye viashiria vya ukatili na kwamba wanaripoti matukio hayo kwa wakati na kisha hatua stahiki huchukuliwa.

“Makosa ya shambulio la aibu,shambulio la kudhuru mwili,shambulio la kawaida,matukio kama haya kwa sasa yamekuwa yakiripotiwa kwa kiasi kikubwa tofauti na zamani baada ya wananchi kuelimika,sababu zamani ilikuwa inaonekana kipigo kwa mila na desturi ni kawaida”.Amesema Kamanda Mark Njera,kamanda wa Polisi Tarime-Rorya.
Wakati huo wito umetolewa kwa viongozi wa kimila,dini,siasa na serikali kutimiza wajibu wao katika kupaza sauti na kukemea vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa watoto,rai ambayo imetolewa na CP Faustine Shilogile ambaye ni Kamishna wa Polisi jamii.

Haya yamejiri wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa jengo la kisasa la Dawati la kijinsia na watoto wilaya ya Tarime,jambo ambalo limepongezwa zaidi na wananchi wa eneo hilo wasema kuwa ni hatua muhimu katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili vilivyokuwa vimekithiri wilayani Tarime na maeneo mengine ya mkoa wa Mara.
“Kwa jengo hili kwa hapa Tarime serikali imetenda haki natamani huduma itakayotolewa hapa isiwe na upendeleo wowote ikiwa mtu ametenda kosa basi sheria ichukue mkondo wake”.Wamesema baadhi ya wakazi wa mji wa Tarime wakati wakizungumza na Tovuti hii.