Na Saada Almasi, Itilima – Simiyu.
Benki ya Dunia (WB) kupitia Shirika la Kazi Duniani (ILO) imetoa Shilingi Milioni 240 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu, kwa ajili ya kulipa vikundi ambavyo vitahusika katika matengenezo ya barabara za Wilaya hiyo.
Meneja Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Itilima, Mhandisi Elgidius Method Kaselwa ameyasema hayo wakati wa kutoa taarifa katika kikao cha baraza la Madiwani cha robo ya nne ya mwaka, kilichoketi Wilayani humo.

Amesema, Halmashauri ya Wilaya ya Itilima imekuwa miongoni mwa wilaya tatu ndani ya Mkoa, ambazo zimepokea fedha hizo na zitatumika kwa vikundi ambavyo ni miongoni mwa vile vilivyosajiliwa katika ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo kufanya marekebisho ya barabara.
Amesema, “hivi vikundi hivi 16 vitafanya kazi za kupunguza uharibifu uliofanyika ndani ya kilometa tano za eneo lao,kwa sababu kuna athari zingine zinatokana na uzembe wa kibinaadamu kama mtu anayechota mchanga ama kokoto kandokando ya barabara na wakati mwingine tunakata miti inaangukia barabarani lakini watu wanakwepa pembeni baadae ule mti unasombwa na maji ya mvua hadi mtaroni mtaro unaziba kesho mtu huyo aliyekata mti atailaumu serikali kwamba barabara mbovu.”
“Hatua ya vile vikundi kufanya zile shughuli katika maeneo yao inakwenda kuwainua watu wengine na kupata uelewa kwamba kumbe tunaweza kuchukua hatua wenyewe pasi na kusubiri serikali ifanye kila kitu,ukizingatia kwamba tumeshapokea tahadhari ya mvua kubwa sasa ili athari isitese jamii ni vema vikundi hivi kufanya kazi hiyo,” alise.a Mhandisi Method.

Wakizungumza na Jambo FM, baadhi ya madiwani mara baada ya kupokea taarifa hiyo wamesema kuwa hatua hiyo si tu inakwenda kusaidia barabara zetu bali itasaidia kuongeza kipato kwa wanakikundi watakaoshiriki.
“Kuna maeneo ambayo unakuta mtu kachota mchanga na watoto wanapita hapo kwenda shule kipindi cha mvua ni hatari sana kwao maji yakipita kwenye huo mkondo na bahati mbaya yakakutana na watoto wadogo ni hatari kubwa wanaweza kusombwa wakafia hapo hivyo ninaamini vikundi hivi vitasaidia sana,” alisema Elizabeth Msingi Diwani Viti Maalum Itilima.
Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Ndolelezi Talange Shashe amesema “ukiachilia mbali fursa ya ajira ambayo wanakwenda kunufaika hivi vikundi pia itakwenda kuwaonyesha watu kuwa kuna vitu hatutakiwa kuililia serikali kwa maana atakapo muona jirani yake mwanakikundi fulani anahangaika na shimo ambalo liko mlangoni kwake kalisababisha yeye kwa uzembe atapata aibu kwamba kesho natakiwa nichukue hatua”.

Naye Mary Ladislaus mkazi wa Lagangabilili ameongea na chombo hiki na kuwataka wakazi wa wilaya hiyo kubadilika na kuacha kulalamika kwa vitu vidogo ambayo si lazima mkono wa serikali ukamilishe
Amesema, “ukiona serikali imefanya kwa upande wake na wewe fikiria utafanya nini kwa upande wako maana hii miundombinu ni yetu tusipoamua kuilinda tutapata tabu sisi wenyewe ,niwaombe wananchi wenzangu wa Itilima tuione hii fursa ya ajira lakini tubadilike kwa kulinda miundombinu yetu.”


