Categories

Do you have a Story?

Call us on 0677 644 444 to submit your news story or incident report!

Mikataba,Mapato na Madeni ni Changamoto Kuu za Sekta Ya Habari Nchini

Imeandikwa na, Ibarahim Rojala

Taarifa ya matokeo ya Kamati ya Kutathmnini hali ya Utendaji wa Uchumi kwenye vyombo vya habari Tanzania Bara iliyokabidhiwa Juni 18,2024 kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan katika Kongamano la Maendeleo ya sekta ya habari Tanzania inaonesha kuwa asilimia 56 ya waandishi wa habari hawana mikataba ya kazi.

Aidha asilimia 38 pekee ya mikataba ya kazi ya Waandishi wa Habari walio na mikataba ya kazi imejumuisha bima ya Afya,asilimia 62 ikiwa haijajumuisha bima hiyo na asilimia 77 ya waandishi wa habari nchini wanalipwa mishahara chini ya Shilingi 500,000 kwa mwezi na baadhi ya vyombo hivyo hulipa kiasi cha shilingi 2,000 kwa kila chapisho la mwandishi.

Tathmini ya ripoti hiyo pia imebaini kushuka kwa mapato ya vyombo vya habari kwa asilimia 50 na zaidi,kupungua kwa nakala za uchapishaji wa magazeti ambapo kampuni tatu za magazeti zimepunguza zaidi ya nakala milioni nne ndani ya kipindi cha mwaka 2020 na 2023 ambayo ni thamani ya Shilingi bilioni nne zilizoondoka katika soko la sekta ndogo ya magazeti.

Sambamba na hayo,wakati tathmini hii ikifanyika,waandishi walikuwa hawajalipwa kwa zaidi ya miezi mitatu,vituo vya utangazaji kushindwa kulipa ada ya leseni ya masafa na wakati mwingine kupitiliza muda mrefu na uwezo mdogo wa kulipa ada ya usambazaji matangazo kwa kampuni zinazosambaza matangazo na uwepo wa mipango ya biashara isiyotekelezeka.

Ripoti inabainisha kwamba sababu kuu za uwepo wa changamoto hizi ni pamoja na uwezo mdogo wa wasimamizi wa vyombo vya habari,usimamizi wa biashara ya vyombo vya habari mabadiliko ya teknolojia na utangazaji na kushuka kwa matangazo kwenye vyombo vya habari.

Sababu nyingine zilizoainishwa kupitia ripoti hiyo ni uwekezaji mdogo kwenye sekta ya habari na utangazaji,uwepo wa wafanyakazi wachache wenye weledi,ujuzi na vipaji vinavyohitajika sokoni,madeni ya vyombo vya habari,mifumo ya kodi na mfumo wa uwekezaji ambapo wageni wanapaswa kuwa na hisa kidogo.

Baada ya kupokea Ripoti hiyo,Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameagiza uchambuzi wa ripoti hiyo kuendelea kufanyika na iwasilishwe serikalini na kueleza kwamba madeni ya serikali yanayodaiwa na vyombo vya habari  yenye ushahidi serikali itahakikisha wyanalipwa.

Pia ameahidi serikali itaangalia namna ya kufanyia marekebisho ya sheria ya uwekezaji kwa wawekezaji ndani ya vyombo vya habari kutoka nje ya nchi,msisitizo wa maudhui salama na kutambua umuhimu wa sekta ya habari katika kukuza demokrasia,uwazi na uwajibikaji na kukemea kashfa na matusi katika uandishi.

Wakati huo huo Rais Dkt.Samia ameziagiza Wizara na Taasisi za Umma kuhakikisha zinafanya malipo ya madeni wanayodaiwa na vyombo vya habari,vyombo vya habari kutoa kipaumbele cha malipo ya mishahara kwa wafanyakazi baada ya kulipwa madeni yao,waandishi kupaza sauti na kuahidi kuwa serikali itasaidia katika eneo la mikataba ya ajira na wizara kuzidisha ubunifu na matumizi ya Teknolojia. Pia amewataka maafisa habari kutoa ushauri kwa viongozi na maafisa wengine serikalini kuhusiana na mbinu bora za mawasiliano na ufikishajiwa taarifa kwa umma na kuhakikisha wanazifahamu sera na vipaumbele vya maeneo yao ya kazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *