MIAKA 20 YA POLISI JAMII: BONANZA LA AMANI, USALAMA LATIKISA KATAVI

Na Daniel Gahu – Katavi.

Wananchi wa Mkoa wa Katavi wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki na kushuhudia kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Polisi Jamii, yanayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi katika kudumisha amani, usalama na umoja wa kitaifa.

Maadhimisho hayo yanafanyika chini ya kaulimbiu “Tushirikiane Kuimarisha Amani, Usalama na Umoja wa Kitaifa,” ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kuzuia uhalifu na kujenga jamii salama kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani (RTO), Leopold Fungu, amesema kaulimbiu hiyo inalenga kuakisi na kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi katika kukabiliana na changamoto za kiusalama kwa njia shirikishi.

Amesema ushirikiano huo unajumuisha mambo mbalimbali, ikiwemo uundwaji na uimarishaji wa vikundi vya ulinzi shirikishi, pamoja na kuimarisha mahusiano ya Polisi Jamii na wananchi.

Kwa mujibu wa Fungu, ushiriki wa wananchi ni nyenzo muhimu katika kuzuia uhalifu, kudumisha amani na usalama, na hatimaye kuwezesha mazingira bora ya maendeleo endelevu ya taifa.

Kwa upande wake, Mrakibu wa Jeshi la Polisi, Superintendent John Mwaipungu, amesema mashindano hayo yamehusisha michezo mbalimbali inayolenga kuwakutanisha askari na wananchi katika mazingira ya kujenga mshikamano na mahusiano mema.

Michezo hiyo inajumuisha mpira wa miguu, netiboli na volleyball, huku mpira wa miguu ukishirikisha timu kutoka katika vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na timu za wananchi.

Amesema burudani hiyo itaendelea hadi siku ya kilele cha maadhimisho, ambapo wananchi watapata fursa ya kushiriki na kushuhudia michezo na mashindano mbalimbali, ikiwemo mchezo wa kukimbiza kuku pamoja na shindano la kunywa mkate na soda.

Katika hatua nyingine, Mgeni Rasmi amewaalika wananchi wote wa Mkoa wa Katavi kujitokeza kwa wingi kwenye bonanza hilo, akisisitiza kuwa michezo hiyo ni sehemu ya kujenga ukaribu na ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.

Aidha, amesema wachezaji watakaoonyesha viwango bora katika mashindano hayo watapata fursa ya kusajiliwa na vikosi vya Jeshi vinavyoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania pamoja na Ligi ya Championship, jambo linalotoa nafasi kwa vipaji vya michezo kutoka Katavi kuonekana na kuendelezwa zaidi.

Kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kufanyika Jumanne, Agosti 25, 2026, katika Viwanja vya Polisi Mpanda, ambapo wananchi watapata fursa ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za michezo, burudani na ujumbe wa kuimarisha amani na usalama.

Maadhimisho hayo ya miaka 20 ya Polisi Jamii yanaendelea kusisitiza dhana kwamba ulinzi na usalama ni jukumu la pamoja, huku ushirikiano wa karibu kati ya Jeshi la Polisi na wananchi ukiwa msingi muhimu katika kuzuia uhalifu, kulinda amani na kujenga jamii yenye mshikamano.


Kaulimbiu: “TUSHIRIKIANE KUIMARISHA AMANI, USALAMA NA UMOJA WA KITAIFA.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *