Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ametowa wito kwa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), ambayo inatimiza miaka 10 ya huduma, kuwa tumaini jipya la kitovu cha ubunifu wa huduma bora za matibabu na utalii wa matibabu, kutokana na uwekezaji mkubwa wa zaidi ya Tsh Bilioni 230, uliowekwa na Serikali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maadhimisho hayo, Senyamule amesema BMH imekuwa tumaini la waliokata tamaa ya magonjwa makubwa.
“Hospitali hii imekuwa ni alama ya mafanikio ya mkoa na Taifa kwa ujumla,” amesema RC Senyamule baada ya kukata utepe kuashiria uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 10 ya kutoa huduma shughuli ambayo itahitimishwa mwezi Februari, mwakani.

Shughuli hiyo imeambatana na kutoa huduma bure za vipimo na matibabu katika viwanja vya vya Nyerere Square, ambapo RC Senyamule ameipongeza Serikali kwa kufanya mapinduzi makubwa ya kuimarisha huduma katika Hospitali hii ya Rufaa ya Kanda ya Kati.
“Hospitali sasa inatoa huduma za ubingwa wa juu 17 na huduma za ubingwa bobezi 20. Huduma hizi zimeokoa sana fedha za kigeni ambazo Serikali ingetumia kwa ajili ya rufaa za nje ya nchi,” amesema Senyamule.
Mkuu wa Mkoa pia ametumia fursa hiyo kuipongeza Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kutoa wauguzi bora wa mwaka kwa mara ya pili mfululizo mwaka uliopita na mwaka huu.

“BMH imekuwa ni moja ya taasisi mahiri za afya nchini na kuleta maendeleo chanya katika sekta ya afya nchini,” ameongeza Bi Senyamule.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof. Abel Makubi amesema mpaka sasa BMH imehudumia wananchi 1.6m toka ianzishwe 2015.
“Kwa sasa, tunahudumia wananchi wagonjwa 1000 mpaka 1200 kwa siku. Dhamira yetu ni kuwa Hospitali ya pili ya Taifa,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali.
Prof. Makubi ameelezea mafanikio makubwa ambayo Hospitali imeyapata kwa muda wa miaka 10 kuwa ni pamoja upandikizaji wa figo kwa wagonjwa 54 na upandikizaji wa uloto kwa watoto 21.


